Ukraine imesema hii leo kwamba vikosi vya Urusi vimesonga mbele upande wa mashariki mwa taifa hilo na kuvikamata vijiji kadhaa katika kile kinachotojwa kuwa kampeni ya Moscow ya kuchukua udhibiti kamili wa jimbo Donbas. 

Wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema jeshi la Urusi limevirudisha nyuma vikosi vya nchi hiyo kutoka maeneo mawili ya jimbo la kaskazini mashariki la Kharkiv na kuikamata miji mingine miwili kwenye mkoa wa Donetsk. 

Taarifa ya wizara hiyo pia imetahadharisha kwamba vikosi vya Urusi vinaendeleza operesheni yake kuelekea vitongoji vingine viwili vya jimbo la katikati mwa Ukraine la Zaporizhzhia (Zapori'ja). 

Mapema mwezi huu Urusi ilisema inaondoa vikosi vyake kutoka karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na kuelekeza nguvu ya kuyakamata majimbo mawili ya Donetsk na Luhansk ikilenga kuunda mpaka kati ya majimbo hayo na rasi ya Bahari Nyeusi upande wa Ukraine.