WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema masuala ya ufuatiliaji na tathmini yanapaswa kupewa kipaumbele ili Taifa liendelee kupata matokeo yanayokusudiwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

“Kwa kufanya hivyo, tutatoa nafasi ya kupima utendaji kwa ujumla na hivyo, kujua tumefikia wapi, tumekwama wapi na wapi tunahitaji kufanya maboresho. Lengo kuu ni kufikia malengo tarajiwa.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo  (Jumatano, Aprili 27, 2022) wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kuwa kongamano hilo linaakisi maono na maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuimarisha tasnia ya ufuatiliaji na tathmini.

Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeandaa mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo unaoainisha majukumu na wajibu wa kila mdau katika usimamizi wa miradi.

Amesema mwongozo huo ambao umesambazwa katika Wizara, Halmashauri na taasisi zote za Serikali utaanza kutumika katika mwaka wa fedha 2022/2023. Mwongozo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi umeainisha umuhimu wa kushirikisha wananchi katika hatua zote za utekelezaji wa miradi.

Amesema ni vyema nchi kuwa na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaotoa fursa ya kushirikisha wananchi na wadau wengine ili kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na sekta binafsi.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wananchi wakiwa na fursa ya kufuatilia na kuhoji utekelezaji wa yale tunayoyaahidi hakika uwajibikaji utaongezeka.

Amesema Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) unachangia kufikia Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063, Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ya mwaka 2050 na Ajenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema bila kuwa na usimamizi madhubuti wa eneo la ufuatiliaji na tathmini itakuwa vigumu kwa nchi yetu kuelewa iko wapi katika utekelezaji wa mipango yote kwa ujumla.

“Kwa kuzingatia kwamba nchi yetu ni sehemu ya Afrika na Dunia, tunaungana na nchi nyingine duniani katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ambayo imepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ikiwemo niliyoitaja hapo juu.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha eneo la Ufuatiliaji na Tathmini linaboreshwa na kusimamiwa ipasavyo.

Amesema mwaka 2008 Serikali kupitia Programu ya Maboresho katika Utumishi wa Umma, iliimarisha eneo la Ufuatiliaji na Tathmni kwa kuboresha miundo ya Wizara zote na kuanzisha Sehemu za Ufuatiliaji na Tathmini chini ya Idara za Sera na Mipango.

“Hii ilikuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha kunakuwepo na ufuatiliaji wa karibu katika utekelezaji wa miradi, kuhakikisha matumizi  ya rasilimali za fedha kwa malengo kusudiwa, kuongeza uwajibikaji na kujifunza kutokana na yale tunayoyatekeleza katika mipango ya kitafaifa.”

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ufuatiliaji na Tathmini (TanEA), Profesa Deus Ngaruko amesema malengo makuu ya taasisi hiyo ni kujenga na kuendeleza uwezo wa ufuatiliaji na tathmini ya ndani ya Serikali na Sekta Binafsi.

Alisema pamoja na mambo mengine, pia kongamano hilo la siku mbili litatoa fursa ya kujifunza mbinu na mambo mapya kwenye tasnia ya ufuatiliaji na tathmini ili Watanzania waweze kujengewa uwezo wa kufanya ufuatilia.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU