Na Benny Mwaipaja, Washington DC
KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.

Bw. Tutuba ametoa rai hiyo mjini Washington DC, Marekani, alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji Dhamana katika Uwekezaji kwa Sekta Binafsi (MIGA), Bw. Junaid Kamal Ahmad.

Alisema kuwa Serikali imeweka vivutio vingi vya uwekezaji ili kuvutia mitaji na teknolojia kutoka nje ya nchi na kuiomba taasisi hiyo itoe dhamana kwa kampuni, taasisi au mashirika yanayotaka kuwekeza nchini Tanzania.

“Tuna maeneo ya uwekezaji kwenye nishati, uendeshaji wa mabasi, reli ya kisasa ambapo wawekezaji wanaweza kuleta vichwa vya treni na mabehewa lakini pia kwenye sekta ya kilimo kwenye miundombinu ya uwagiliaji, pamoja na uwekezaji kwenye sekta ya utalii kwa kujenga hoteli za kisasa na miundombinu mingine” alisema Bw. Tutuba

Bw. Tutuba alisema kuwa MIGA inatakiwa kutoa dhamana kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu na wawekeze kwenye maeneo hayo.

Alisema kuwa Tanzania imeialika Taasisi hiyo kufanya majadiliano ya pamoja na wawekezaji kutoka pembe zote za dunia mwezi Julai, 2022 nchini Tanzania, hatua itakayochochea masuala ya uwekezaji ambao lengo lake ni kukuza uchumi wa nchi, ajira na hatimaye kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja.

“Kikao kimekuwa na mafanikio makubwa kama watakuja na kutoa dhamana kwa wafanyabiashara wa ndani, ninaamini wafanyabiashara wa chini watakuwa wa kati na wa kati watakuwa wafanyabiashara wakubwa ambao uwekezaji wao utazalisha ajira, kukuza uchumi na kuchangia mapato na kodi nyingine za Serikali na kuongeza kipato cha mtanzania mmoja mmoja” alisema Bw. Tutuba

Kwa upande wake, Makamu wa Rais anayesimamia masuala ya uendeshaji wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji Dhamana katika Uwekezaji kwa Sekta Binafsi (MIGA), Bw. Junaid Kamal Ahmad, aliipongeza Tanzania kwa hatua zake za kuboresha mazingira ya uwekezaji ambayo anaamini yatavutia wawekezaji wengi kuwekeza nchini humo.

Alisema kuwa Taasisi yake iko tayari kufanya mkutano wa majadiliano na wadau wa sekta binafsi nchini Tanzania na kuahidi kuendelea kuwashawishi wawekezaji wengi kwenda kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati pamoja na maeneo mengine yatakayochangia kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na maisha ya  watanzania.

Alisema kuwa Sekta Binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi wan chi yoyote duniani na kwamba mazingira mazuri ya uwekezaji ynyofanywa na Tanzania yatasababisha wawekezaji wengi kufulika nchini humo na kwamba watatumia mkutano huo wa majadiliano kuchadili furs ana changamoto za uwekezaji huo na kuzipatia ufumbuzi wa Pamoja.