Tanzania Na Kenya Kuendelea Awamu Ya Pili Uimarishaji Mpaka
Na Munir Shemweta, WANMM TARIME
Tanzania na Kenya zimetia saini makubaliano ya Mpango Kazi wa kuendelea na kazi ya Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizo kutoka eneo la Ziwa Natron hadi Namanga mkoani Arusha.
Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Wataalamu wa Mipaka kati ya nchi hizo kilichokuwa na lengo la kupokea mawasilisho ya utekekezaji kazi za awamu ya kwanza na kuangalia namna bora ya kukamilisha awamu ya pili.
Utiaji saini ulifanyika tarehe 14 April 2022 wilayani Tarime mkoa wa Mara kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor na Bi. Juster Nkoroi ambaye ni Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO).
Mbali na utiaji saini makubaliano ya Mpango Kazi, Kamati ya Wataalamu wa mipaka wa nchi za Kenya na Tanzania ilitembelea mpaka wa nchi hizo maeneo ya Kirongwe wilayani Rorya kwa upande wa Tanzania na Muhuru Bay katika Kaunti ya Migori nchini Kenya pamoja na mpaka wa nchi hizo eneo la Serengeti/Masai Mara ili kukagua kazi ya uwandani na kushauri namna bora ya kuendelea na kazi zinazofuta.
Awamu ya kwanza ya uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo ulikuwa wa kipande cha urefu wa Km 238 kuanzia Ziwa Victoria hadi Natron ambapo awamu hiyo ilikamilishwa hivi karibuni kwa kipande cha Km 23 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara hadi Ziwa Natron.
Katika makubaliano ya Mpango Kazi, utekelezaji Uimarishajji Mpaka wa Tanzania na Kenya awamu ya pili utaanza mwishoni mwa mwezi April 2022 na kutarajiwa kukamilika Juni 2022 kwa kipande cha Km 110 kutoka Ziwa Natron Hadi Namanga mkoani Arusha kufanyiwa kazi.
Wakati wa utiaji saini makubaliano ya Mpango Kazi viogozi wote wawili walihimiza wataalamu wa mipaka watakaoshiriki zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kuondoa tofauti zao wakati wa utekelezaji kazi hiyo na kusisitiza kuwa uimarishaji ulenge kudumisha mahusiano mazuri na kuleta manufaa kwa Tanzania na Kenya.
Mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la nchi kavu una ukubwa wa Km 758 na uimarishaji wake pamoja na mambo mengine utasaidia kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikijotokeza kwa wananchi wanaofanya shughuli maeneo ya mipakani katika nchi hizo.