Na Benny Mwaipaja, Washington DC
Nchi za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimewasilisha maombi ya kupatiwa mkopo wenye masharti nafuu kwenye Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza-Msongati- Gitega, yenye urefu wa Km 939, uliokisiwa kugharimu dola za Marekani milioni 900.

Majadiliano ya awali kati ya Benki hiyo na Mawaziri wa Fedha wa Nchi hizo tatu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba wa Tanzania, Mhe. Nicolous Kazadi wa DRC na Mhe. Dkt. Domitien Ndihokubwayo wa Burundi, yamefanyika Washington DC, kando ya Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, Washington DC, nchini Marekani.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa reli hiyo ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya kiuchumi ya nchi zote tatu kwa sababu itakapokamilika itarahisha usafirishaji wa mizigo, abiria na kukuza biashara na maendeleo ya viwanda ya nchi hizo.

Alisema kuwa mradi huo ni mkubwa ndiyo maana nchi hizo zimekubaliana kutafuta mikopo nafuu kutoka vyanzo mbalimbali na pia kwa kutumia fedha zitakazotengwa kwenye bajeti zao za ndani ili mradi huo uanze kujengwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Nnenna Nwabufo, alisema kuwa Benki yake inatambua umuhimu wa mradi huo kiuchumi, kisiasa na kijamii na kwamba utasaidia pia kuziunganisha nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ni muhimu kwa ajili ya utengamano wa nchi hizo.

Aliahidi kuwa Benki yake itashiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa mradi huo unajengwa kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo pamoja na maendeleo ya kiuchumi ya nchi zinazoshiriki katika kujenga mradi huo muhimu.

Mwisho