Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali imedhamiria kutenga Mfuko maalum kwa ajili ya kudhibiti upandaji wa bei za pembejeo ikiwemo mbolea na bei za mazao ili kuhakikisha wanapunguza maumivu kwa Wakulima kwa kuwawekea bei rafiki kwa katika shughuli zao.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbeya Vijijini, Mhe. Oran Manase Njeza lililohoji kuhusu mpango wa Serikali kuhakikisha wanarudisha ruzuku kama ilivyo kwa nchi zingine za Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Afrika.

Akizungumza kuhusu mkakati wa Serikali wa kupunguza bei za mbolea zinazopanda kwa kasi kubwa kwenye soko la Dunia, Naibu Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali imeanza kuchukuwa hatua za haraka, za muda wa kati na muda mrefu katika kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ambapo hatua za haraka ni pamoja na kudhibiti upandaji holela wa bei usiozingatia gharama halisi za uingizaji wa mbolea nchini kwa kutangaza bei elekezi zinazopaswa kuzingatiwa na wafanyabiashara katika maeneo ya uzalishaji.

Amefafanua kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona viwanda vingi vya mbolea vinajengwa nchini ili kuongeza upatikanaji wa mbolea na kupunguza bei ya mbolea kama ilivyo hivi sasa ambapo moja kati ya mikakati iliyokuwepo ni kukaribisha Wawekezaji wengi zaidi wa viwanda vya mbolea ili kwa pamoja tuweze kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea.

“Serikali imekutana na uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto za kiwanda ili kuhakikisha kinaongeza Uzalishaji wa mbolea kutoka wastani wa tani 30,000 hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka, tunaamini ongezeko la uzalishaji wa mbolea utasaidia kuongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo na kusababisha bei kuwa nzuri”, alisema Mhe. Mavunde.

Serikali imepata wawekezaji wapya wa viwanda vya mbolea ambapo kampuni ya Itracom Fertilizers Limited kutoka Burundi imejitokeza na inajenga kiwanda katika Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka.