Serikali imesema wiki ijayo itatangaza nafasi za ajira 32,000 katika sekta ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi.
Ahadi hiyo imetolewa Bungeni leo Jumatano Aprili 6, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama ambapo amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kuajiri .
Waziri Mhagama ametoa majibu hayo yaliyotokana na maswali mengi ya nyongeza na wabunge yaliyoulizwa katika Wizara ya Tamisemi wakitaka kujua namna ambavyo Serikali itapeleka watumishi kuziba nafasi katika vituo vingi vilivyojengwa nchini.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini Serikali ilipanga kuajiri watumishi 44,000 kwa mwaka huu wa fedha, na tayari tumeshaajiri watumishi 12,000 na sasa nitangaze kuwa wiki ijayo nitatangaza ajira 32,000,” amesema Mhagama.
Awali Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde amesema wizara hiyo ingetoa tangazo la ajira na mgawanyiko wake na kuomba wabunge kuwa watulivu.