WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini na iko tayari kuwawezesha wawekezaji kutoka ndani na nje wenye nia ya kuwekeza nchini.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo  wakati  alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Mhe. Donald Wright  kuhusu fursa za uwekezaji na ufanyaji biashara zilizopo Tanzania  pamoja na kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma Aprili 05, 2022.

Akiwa ameambata na Viongozi wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara akiwemo Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara, Naibu Katibu Mkuu  Bw. Ally Gugu, Dkt. Kijaji amemhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali iko tayari kuwawezesha wawekezaji kutoka Marekani katika maeneo ya  uzalishaji wa Mbolea na mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo kama ngano, mafuta ya kula na sukari ili kuondoa upungufu uliopo nchini.

Naye Balozi huyo wa Marekani nchini Tanzania amesema Marekani itaendelea kuwekeza na kufanya biashara nchini katika maeneo ya kilimo biashara, uchumi wa blue, uchakataji wa mazao, uwezeshaji vikundi vya wanawake wajasiriamali pamoja na kuandaa maonesho na makongamano mbalimbali yanayolenga kuhamasisha na kukuza biashara nchini.