NA. MWANDISHI WETU

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kapar Mmuya amesema Serikali imedhamiria kutokomeza tatizo la utapiamlo nchin ili kuendelea kuwa na jamii yenye afya njema kwa maendeleo ya nchi.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utekelezaji wa afua za Lishe mkoani Morogoro kwa lengo la kujionea na kutatua changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji huo ambapo alifanikiwa kutembelea shughuli za uzalishaji kwa wamiliki wa viwanda vidogo na vya kati vinavyochakata unga wa lishe ikiwemo cha Kala Investment na kiwanda cha unga wa sembe cha Asante Mungu  pamoja na kutembelea miradi ya lishe ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.

Naibu Katibu Mkuu alisema Serikali imedhamiria kukabili changamoto zitokanazo na ukosefu wa lishe bora nchini ikiwemo tatizo la utapiamlo, udumavu, ukondefu na upungufu wa damu kwa wajawazito na watoto katika jamii zetu.

“Kama nchi tumepiga hatua ya kupunguza tatizo la utapiamlo kwa kuzingatia tafiti iliyofanywa mwaka 2018 na 2019 ulibaini kuwa tumetoka  asilimia 3.8 na kufikia asilimia 3.5 pamoja na kupunguza tatizo la udumavu kutoka asilimia 34 hadi 31. 8”.alieleza Mmuya.

Pamoja na hayo alieleza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za wadau mbalimbali wanaoshughulikia masuala ya lishe nchini kwa kuhakikisha mazingira ya utekelezaji wa shughuli zao yanakuwa rafiki.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya mahusiano baina ya wadau na Serikali kutoka kampuni ya SANKU project healthy Children Bw. Omari Gwao aliishukuru Serikali kwa kuimarisha ushirikiano uliopo baina yao huku aieleza mikakati yao katika kusaidia masuala ya lishe.

“Kwa kushirikiana na Serikali tunasaidia wazalishaji wadogo na wakati kwa kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi ikiwa ni afua mojawapo ya kupambana na utapiamlo nchini,”alisema Bw. Gwao

Kazi kubwa ni kuisaidia Serikali kufikia malengo yake ya kupambana na changamoto za lishe duni kwa kuwasaidia wazalishaji wadogo wadogo na wakati kwa kuwapatia kinyunyizi kinachoitwa dosifier kinachotumika kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi.

“Hadi sasa SANKU inafanya kazi katika mikoa yote ya Tanzania na tayari tumezifikia Wilaya 102 na tumeweza kushirikiana na wazalishaji zaidi ya 700 lengo likiwa kuwafikia wazalishaji zaidi ya 1000 ili kusaidia kupambana na masuala ya utapiamlo nchini,”alisisitiza Gwao.

 Aliongezea kuwa, wanajivunia mkoa wa Morogoro kwani hadi sasa wamewafikia wazalishaji 115 na kumekuwa na matokeo makubwa kwa kuboresha maeneo ya wazalishaji, kwa kuzingatia tafiti zilizofanywa juu ya masuala ya lishe mkoa ulikuwa wa 25 na hadi sasa umefikia nafasi ya 5 na hii ni moja ya mafanikio kwao,”aliongezea.

Naye Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Bw. Selestine Martine alisema hali ya uelewa wa masuala ya lishe kwa Watanzania imeongezeka kwa kulinganisha miaka ya nyuma ambapo kumekuwa na ongezeko la watu wanaotumia lishe bora.

“Jamii imekuwa na muamko wa kula vyakula kwa kuchanganya makundi mbalimbli hii inatia moyo na kuona jamii imeendelea kupata elimu na kuzitumia kuhakikisha tunakuwa na watu wenye afya njema,”alisema Martine.

 

=MWISHO=