Sarafu za Euro na Pound ya Uingereza zimeporomoka thamani yake baada ya Russia kuamua kuzikatia gesi nchi za Poland na Bulgaria

Hayo yameripotiwa na televisheni ya Euro News ambayo imesema kuwa, sarafu ya Euro imeporomoka mbele ya dola ya Marekani baada ya Russia kuzikatia gesi Poland na Bulgaria. Thamani ya Euro imeporomoka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Pound ya Uingereza pia imeporomoka mbele ya sarafu ya dola kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita baada ya Russia kuamua kusimamisha kupeleka gesi yake katika nchi mbili za Poland na Bulgaria za mashariki mwa Ulaya.

Bei ya gesi katika nchi za Ulaya jana Jumatano iliongezeka kwa zaidi ya asilimia 23 baada ya kuchukuliwa hatua hiyo ya Russia ikiwa ni kujibu vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow.
Nchi za Ulaya ni tegemezi mno kwa nishati ya Russia

Hatua hiyo ya Russia imechukuliwa baada ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia kusema kuwa nchi za Magharibi zinachuana kutuma silaha Ukraine. Maria Zakharova ameashiria madai ya nchi za Magharibi kwamba zinafanya juhudi kurejesha amani huko Ukraine na kusisitiza kuwa: "Hatua hii ya Magharibi inakinzana na matamshi ya nchi hizo."

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa, nchi za Magharibi zinafanya kila kinachowezekana ili kuchelewesha oparesheni amilifu ya jeshi la Russia nchini Ukraine.

Ikumbukwe kuwa, juzi Jumanne, Christine Lambrecht Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani alisema kuwa, Berlin itatoa kibali cha kuikabidhi Ukraine vifaru; hatua inayodhihirisha kubadilika wazi sera za tahadhari za Berlin katika suala la kuiunga mkono kijeshi serikali ya Kiev.