Rais Vladimir Putin wa Russia amewaagiza wanajeshi wa nchi hiyo kutovamia ngome ya mwisho ya Ukraine iliyosalia katika mji uliozingirwa wa Mariupol badala yake wauzingire mji huo ili hata nzi ashindwe kuingia katika mji huo.

Rais Vladimir Putin wa Russia ameeleza hayo katika mazungumzo yake na Sergei Shoigu, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Waziri wa Ulinzi wa Russia amesema kuwa sehemu iliyosalia ya mji wa Mariupol ambayo kwa kiasi kikubwa iliharibiwa kwa mashambulizi ya mabomu tayari imekombolewa isipokuwa kiwanda kikubwa cha chuma cha Azovstal ambapo wanajeshi wa Ukraine waliobaki walikuwa wakiendelea kushikiliwa eneo hilo.

Rais Putin ameongeza kuwa, uamuzi wake wa kusitisha mashambulizi dhidi ya kiwanda hicho cha chuma ni kwa lengo la kuwalinda wanajeshi wa Russia na amepongeza oparesheni hiyo kuwa ni ya mafanikio.

Waziri wa Ulinzi wa Russia pia amesema kuwa wanajeshi wa nchi hiyo wamefanikiwa kukizingira salama salimini kiwanda hicho cha kuzalisha chuma huko Mariupol na kwamba kukiacha kiwanda hicho mikononi mwa wanajeshi wa Ukraine kunawakwamisha wenzao wa Russia kutangaza ushindi kamili huko Mariupol; mji ambao umeshuhudia mapigano makali.  Udhibiti wa majeshi ya Russia katika mji huo umetajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa upande wa kistatijia.