Mradi Wa Majitaka Wa Euro Milioni 5.3 Kujengwa Mkoani Mwanza
Na Mohamed Saif- Mwanza
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) inatarajia kutekeleza ujenzi wa mradi wa miundombinu ya majitaka na usafi wa mazingira wenye thamani ya Euro Milioni 5.3 kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria.
Mradi huo unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya uratibu wa LVBC kupitia programu ya Pamoja ya Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRM).
Hayo yalibainika hivi karibuni Jijini Mwanza katika kikao kilichoshirikisha wadau kutoka MWAUWASA, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) ukiongozwa na Meneja anayesimamia miradi Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, Martina Maurer.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele alisema ufadhili huo uliweka vipaumbele mbalimbali vyenye nia ya uhifadhi wa mazingira kwa miji inayozunguka Ziwa Victoria kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Mradi utawezesha ukarabati na upanuzi wa mtandao wa majitaka kwa takriban kilomita 14.4 sambamba na kuunganisha kaya 1,600, uboreshaji vituo vya kusukuma majitaka na ununuzi wa vifaa vya usimamizi wa Mfumo wa Majitaka yakiwemo magari ya kuondoa taka majumbani,” alibainisha Mhandisi Msenyele.
Mhandisi Msenyele alisema ufadhili huo unafuatia ushirikiano madhubuti baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan na mataifa ya nje. “Wengi ni mashahidi, mnaona namna ambavyo Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan anavyoweka msisitizo kwenye suala la ushirikiano wa kimataifa,” alisema Mhandisi Msenyele.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa kwenye utunzaji wa Mazingira hususan kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria. “Mradi huu utasaidia kuwaondolea adha wananchi ya kujaa mara kwa mara kwa mashimo ya vyoo na hii itapunguza uchavuzi wa Ziwa letu,” alisema Mhandisi Msenyele.
Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni Meneja wa Benki ya KfW upande wa Afrika, Martina Maurer alisema mradi umelenga kupunguza uchafuzi wa Ziwa Victoria hususan unaotokana na utiririshaji ovyo wa majitaka.
Akielezea kuhusiana na ziara yao hiyo ya siku moja Mkoani Mwanza, Maurer alisema imelenga kujionea eneo la mradi na kujadili namna bora ya utekelezwaji wake.
“Tunatarajia kujifunza mengi kuhusu namna mnavyotekeleza miradi yenu hususan ya utunzaji wa mazingira (uondoshaji wa majitaka) sambamba na kujadili changamoto zinazowakabili kwenye utekelezaji wa miradi kwa ufumbuzi wa pamoja na pia kubaini maeneo zaidi tunayoweza kushirikiana,” alisema Maurer.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Kaimu Meneja Ufundi wa MWAUWASA, Mhandisi Salim Lossindilo alitaja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Igogo, Kirumba, Mwaloni, Nyamanoro, Kitangiri na Pasiansi.
Mhandisi Lossindilo vilevile alitaja maeneo kadhaa ya ushirikiano ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya majitaka kwenye eneo linalozungukwa na Mto Mirongo ambapo alisema wanatarajia kuunganisha wananchi wapatao 100,000 na mfumo wa majitaka ili kupunguza uchafuzi wa mto huo.
“Tumeandaa maandiko matano ya miradi itakayonufaisha Wilaya za Ilemela na Nyamagana yenye lengo la kutunza Ziwa Victoria na inashirikisha Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela, Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria pamoja na MWAUWASA,” alibainisha Mhandisi Lossindilo
Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea maeneo yatakayonufaika na mradi huo wa Uwekezaji wa Kipaumbele cha Juu (HPI-areas), mabwawa ya majitaka ya Butuja na mradi rahisi wa uondoshaji majitaka maeneo ya milimani (Simplified Sewerage System).
Kwa nyakati tofauti ujumbe huo uliipongeza MWAUWASA kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na hususan wa maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.