Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Extra-Ordinary Ministerial Committee of the Organ) ambao utahusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) utafanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.

Mkutano huo ambao umetanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu (Senior Officials meeting), unalenga pamoja na mambo mengine Kupokea na Kujadili Ripoti ya Maendeleo ya Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) pamoja na Mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Makatibu Wakuu.

Itakumbukwa kuwa, wakati wa Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulichofanyika jijini Maputo, Msumbiji mwezi Juni 2021, uliridhia kupelekwa kwa Misheni ya SAMIM (SADC Mission in Mozambique) nchini Msumbiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo kupamabana na ugaidi na vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto vilivyokuwa vinaendelea kwenye baadhi ya Wilaya zilizopo kwenye Jimbo la Cabo Delgado.

Misheni hiyo ambayo ilianza kazi rasmi mwezi Julai 2021, inajumuisha Nchi Wanachama kumi (10) za SADC ambazo ni Tanzania, Angola, Malawi, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Botswana, Zimbabwe na Zambia.

Lengo kuu la misheni hiyo ni kukomesha matishio ya ugaidi, kuimarisha hali ya ulinzi na usalama, kurejesha utawala wa sheria kwenye maeneo yaliyoathirika kwenye Jimbo la Cabo Delgado na kuisadia Msumbiji kwa kushirikiana na Mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu ili kuyawezesha kutoa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika na vitendo vya kigaidi ikiwemo kuwasaidia watu walioyakimbia makazi yao.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo utaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. Viongozi wengine kutoka Tanzania watakaoshiriki Mkutano huo ni pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.