Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kukamilisha uchunguzi wa miradi 52 ya maendeleo  ambayo haikuzinduliwa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa  mwaka 2021.

Akizungumza jana mkoani Njombe wakati akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alisema kuwa TAKUKURU wanatakiwa kuhakikisha wanakamilisha miradi iliyokuwa imekataliwa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 baada ya kukutwa na dosari.

“TAKUKURU katekelezeni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kukamilisha uchunguzi wa miradi 52 iliyokuwa na dosari na haikuzinduliwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 na endapo kuna ushahidi wa kutosha basi waliohusika  muwafikishe Mahakamani” Alisema Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango.

Aidha, aliwataka wanaokimbiza Mbio za Mwenge kwa mwaka huu kuhakikisha wanakagua na kuzindua miradi ya maendeleo iliyo katika viwango vinavyotakiwa.

“Hakikisheni miradi mtakayozindua inalingana na thamani ya fedha iliyotumika na endapo kutakuwa na changamoto toeni taarifa katika mamlaka inayohusika ili miradi hiyo ifanyiwe uchunguzi.” Alisisitiza Makamu wa Rais.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango ameiagiza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kuendelea na mipango na mikakati yake ya kudhibiti na kuzuia dawa hizo nchini.

“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya endeleeni na operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya kwenye maeneo ya mipakani  na nasisistiza muwe mnakamilisha uchunguzi na kuchukua hatua za nidhamu kwa wote wanaohusika” Alisisiza Makamu wa Rais.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa baada ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 vijana sita waliondaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, wataukimbiza Mwenge wa Uhuru katika mikoa 31 na halmashauri 195 nchini kwa siku 195.

Aidha, Prof. Ndalichako alisema kuwa kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, ugonjwa UKIMWI pamoja na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na Malaria.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 zitafikia kilele chake Oktoba 14, 2022 mkoani Kagera zenye kauli mbiu Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa ikiwa ni ujumbe uliozingatia hoja na vipaumbele vya Serikali ikiwemo umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 itakayofanyika Agosti 14, 2022.


Mwisho.