Majaliwa: Miundombinu Imara Ni Chachu Ya Ukuaji Wa Uchumi
MIUNDOMBIU imara ya usafiri na usafirishaji ni kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi kwani mbali na kutumika kama kivutio kikubwa cha uwekezaji, ukuaji wa biashara, utalii na kilimo pia inarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama afya na elimu.
Ni ukweli usiopingika kwamba Taifa lolote duniani lenye nia na dhamira ya dhati ya kujiletea maendeleo katika sekta mbalimbali halina budi kuwekeza ipasavyo kwenye sekta hii mtambuka ya usafiri na usafirishaji.
Novemba 26, 2016 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon aliwahi kusema kuwa sekta ya usafiri na usafirishaji ni chanzo kikubwa cha ajira na injini ya ukuaji wa uchumi na alisisitiza kuwa suala hili lazima liwe endelevu ili kufikia jamii vijijini.
“Usafirishaji endelevu unaweza kusaidia kuleta ajira, kupunguza umaskini, kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika, kuwawezesha wanawake na kukuza ustawi wa makundi mengine katika mazingira magumu,” alisema.
Kwa msingi huo, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha miundombinu na huduma za usafirishaji ili kupunguza gharama za uzalishaji na kufanikisha maendeleo ya nchi kwa haraka sambamba na kutumia fursa za kijiografia kuinua uchumi wetu.
Akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ili iweze kuleta tija zaidi.
Akizungumzia miundombinu ya barabara na madaraja, Mheshimiwa Majaliwa alisema katika mwaka 2021/2022, Serikali imejenga jumla ya kilomita 251.9 za barabara kwa kiwango cha lami ambazo zimehusisha barabara kuu, barabara za mikoa na wilaya.
Mheshimiwa Majaliwa alisema lengo ujenzi wa barabara hizo ni kuhakikisha kuwa makao makuu ya mikoa yote na nchi jirani zinaunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na mizigo.
Alisema Serikali imeanza awamu ya pili ya ujenzi wa barabara na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam na ujenzi wa barabara za mchepuo (bypass) katika Jiji la Mbeya, Dodoma na Mji wa Iringa.
Aidha, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa barabara za mchepuo katika majiji ya Mwanza na Arusha umekamilika. “Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa kilomita 19.2 ambayo imekamilika kwa asilimia 86 (baada ya nyongeza za kazi za mkataba) na barabara za juu katika eneo la Keko na Kurasini.”
Waziri Mkuu amesema mbali ya ujenzi wa barabara pia Serikali imedhamiria kuboresha usafiri wa anga kwa kuwa usafiri huo ni muhimu katika kuongeza tija na ufanisi katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa kukarabati viwanja vya ndege, ujenzi wa viwanja vipya vya ndege pamoja na ununuzi wa ndege mpya.
Alisema Serikali katika mwaka 2021/2022 imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili liweze kutoa huduma bora ya usafiri wa anga ndani na nje ya nchi. “Hadi Februari, 2022, Serikali imefanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege tano mpya.”
Alisema kati ya hizo, ndege moja ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner; ndege mbili aina ya Boeing 737-9; ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400; na ndege moja ya mizigo aina ya Boeing 767-300F. Kukamilika kwa ununuzi wa ndege hizo, kutaiwezesha Serikali kuwa na ndege mpya 16.
Pia, Waziri Mkuu aliongeza kuwa kutokana na kuendelea kuimarika kwa shirika la ndege, hivi karibuni limefanikiwa kuanza safari katika vituo vya Arusha, Geita, na kurejesha safari za Mtwara na Songea.
Aidha, Waziri Mkuu alisema mbali na kuanza safari katika mikoa hiyo pia, shirika hilo limerudisha safari za kikanda katika vituo vya Bujumbura, Entebbe, Harare, Lusaka na Hahaya pamoja na kuanzisha vituo vipya vitatu katika miji ya Lubumbashi, Nairobi na Ndola.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa Shirika la Ndege Tanzania limefanikiwa kurejesha safari ya kimataifa kwenda Mumbai – India pamoja na kuanzisha safari za mizigo kuelekea Guangzhou – China.
Aidha, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu miundombinu ya reli, ambapo alisema pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika mwaka 2021/2022, Serikali imeendelea na ukarabati wa njia ya Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma sambamba na ununuzi wa vichwa vya treni vitatu, mabehewa 44 ya mizigo na mtambo wa kupima ubora wa njia ya reli.
Alisema katika mwaka 2022/2023, kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuendelea kutafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli kwa kipande cha Tabora – Isaka (Km 165) na ujenzi wa njia za reli kwa vipande vya Uvinza – Musongati – Gitega (Burundi) yenye urefu wa Km 282; na Kaliua – Mpanda – Karema (Km 321) kwa kiwango cha SGR.
Kuhusu miundombinu ya bandari, Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza mpango wa uboreshaji wa bandari nchini kwa kufanya upanuzi na kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Alisema katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha ukarabati wa gati nambari 1-7 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza kina hadi kufikia mita 14.5. Aidha, gati maalum la kuhudumia meli za magari limeanza kutumika na kazi ya kuchimba na kupanua lango la kuingilia meli bandarini na sehemu ya kugeuzia meli inaendelea na ujenzi wake umefikia asilimia 15.
“Vilevile, Serikali imeendelea kuboresha Bandari za Tanga na Mtwara ambapo kazi ya uongezaji wa kina cha lango la kuingilia meli kutoka mita nne hadi mita 13 pamoja na kuweka vifaa vya kuongozea meli katika Bandari ya Tanga umekamilika. Utekelezaji wa awamu ya pili ya uboreshaji wa Bandari ya Tanga umefikia asilimia 25.”
Waziri Mkuu alisema Serikali inatarajia kununua vivuko vipya vitano katika mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kutoa huduma katika maeneo ya Kisorya – Rugezi, Ijinga – Kahangala, Bwiro – Bukondo, Nyakarilo – Kome, Nyamisati – Mafia na kivuko kipya cha Magogoni – Kigamboni pamoja na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu muhimu ya usafiri na usafirishaji.
Mbali na maboresho katika sekta ya bandari, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano kwa kupanua mtandao wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano nchini na katika nchi jirani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Alisema mwaka 2021/2022, Serikali imejenga kilomita 409 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufikia urefu wa kilomita 8,319 sawa na asilimia 55 ya lengo la kufikia kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa Serikali imefanikiwa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi ya Msumbiji kutokea eneo la Mangaka hadi Mtambaswala, hatua ambayo imefanya nchi zilizounganishwa na Mkongo wa Taifa kufikia saba ambazo ni Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Msumbiji, Malawi na Zambia.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaunganishwa kupitia Ziwa Tanganyika na hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mawasiliano katika Ukanda wa Maziwa Makuu kuelekea uchumi wa kidijitali.