Bandari ya Dar es Salaam imeandika historia mpya baada ya kupokea kwa mara moja magari 4,041.

Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya meli iliyobeba magari hayo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema tangu kukarabatiwa kwa gati namba 1 hadi 7 iliyogharimu Trioni moja imesaidia kuongeza idadi ya magari yaliyokuwa yakishushwa kutoka magari 700 hadi 4000 na zaidi kwa siku.

Profesa Mbarawa amesisitiza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa magari yote yanayoagizwa kukaguliwa huko yanakotoka yakifika Tanzania yatoke bila kukaguliwa ili kuepuka msongamano wa magari bandarini.

“Nataka nisisitize agizo la Rais wetu kuwa magari yote yakaguliwe huko huko yanakotoka kuepuka msongamano wa magari bandarini na niwatake mamlaka ya bandari kuwa na timu ya masoko iende huko nchi zingine kuitangaza bandari yetu kwa huduma bora inazotoa hasa usalama wa bandari yetu” amesema Profesa Mbarawa

Aidha Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi amesema gari hizo zilizoshushwa leo gari 1105 sawa na asilimia 27% ni za hapa nchini na gari 2936 sawa na asilimia 73% zinakwenda nchi jirani kama Sudan Kusini, Zimbabwe, Msumbiji na Malawi

Eric ameongeza kuanzia tarehe 5 hadi 7 Aprili (Siku tatu) wamepokea meli nne zenye jumla ya magari 8384 ukilinganisha na mwaka uliopita walikuwa wakipokea gari 10,000 kwa mwezi mmoja

“Meli hii imetumia muda wa siku 19 ikitoka Japan hadi Tanzania ukilinganisha na kipindi cha nyuma meli ilikuwa ikitumia siku 40 na niseme meli zingine mbili zitaingia mwezi huu Aprili zikiwa na jumla ya magari 2000”