Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza nauli mpya za mabasi ya mijini maarufu daladala na mabasi ya masafa marefu.

Akitangaza kiwango hicho kipya cha nauli  Jumamosi Aprili 30, 2022 Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe amesema kiwango hicho kipya kitaanza kutumika baada ya siku 14.

Amesema kwa mabasi ya mjini kuanzia Kilomita 0 hadi 10 nauli itakuwa Sh500 badala ya 400 na nauli ya Sh450 itakuwa ni 550.

"Kwa kilomita 30 nauli itakuwa 850 badala ya 750 na kwa kiliometa 35 nauli itakuwa 1000 na kwa huku kwa upande wa Kilometa 40 nauli itakuwa 1100" amesema Ngewe

Amesema kwa mabasi ya mkoani daraja la kawaida kwa kwa Kilometa 1 imeongezeka kwa asilimia 11 kutoka Sh 36 kwa kilometa moja hadi Sh41.

"Kwa daraja la kati imeongezeka kwa asilimia 6 abiria mmoja atalipa Sh56.88 kwa kilometa kutoka Sh53" amesema.