Korea Kaskazini imefanya jaribio jingine la aina mpya ya makombora katika tukio ambalo limeshuhudiwa na kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong Un, usiku wa kuamkia leo.
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kaskazini ambalo limezitaja silaha hizo mpya kuwa za kisasa na zinazoongeza uwezo wa nchi hiyo katika medani ya vita vya nyuklia. Baada ya kusimamia jaribio hilo la leo,
Kim Jong Un ametoa maelekezo ya kuimarishwa kwa uwezo wa ulinzi na nguvu za nyuklia nchini mwake.
Jeshi la taifa jirani la Korea Kusini limesema limebaini kurushwa kwa makombora mawili kutoka pwani ya mashariki ya Korea Kaskazini yaliyosafiri umbali wa kilomita 110.
Taarifa za jaribio hilo zimetolewa katika wakati kuna ishara kwamba hivi karibuni Korea Kaskazini inaweza kuanza tena majaribio yake ya silaha za nyuklia baada ya Pyongyang kukiuka marufuku ya kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu mwezi uliopita.