Kinana Ataka Waliotajwa Ripoti Ya Cag Hatua Zichukuliwe
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ametoa ushauri kwa Serikali kuhakikisha wote waliotajwa kufuja fedha za umma kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) wanachukuliwa hatua.
Amesema haina maana kila mwaka ripoti ya CAG inatolewa halafu hakuna hatua ambazo zinachukuliwa dhidi ya wahusika wote ambao wametajwa, hivyo umefika wakati sasa kuchukua hatua ili kukomesha ufujaji wa fedha za umma.
“Kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kinyume na utaratibu, niwoambe wenzangu serikali, ni wakati muafaka watu waliotajwa, waliohusika, waliotenda, walioshiriki kwa namna moja au nyingine wachukuliwe hatua.
“Kila mwaka ripoti ya CAG inapotolewa wabunge wamekuwa wakijadilia na baada ya kujadili inakuwa nini? Haitoshi hatua zikichuliwa hali inakuwa tofauti , wabunge wanazungumza kwa ukali kabisa, taarifa inaandika halafu inakuwa imekwisha.
“Mwaka unaofuata mambo ni yale yale, wizi ni ule ule, ingekuwa hatua zinachukuliwa papo kwa papo haya mambo yangeisha.Watu wangechukua wanachukuliwa hatua wangechukua tahadhari, waliohusika waondolewe na watu wa kujaza hizo nafasi wapo.
“Wakati umefika kwa Serikali kufanyia kazi kwa kina ripoti ya CAG ili wananchi waridhike mali ya umma haitumiki vibaya.Mnaunga mkono au tuwahurumie, haiwezekani vitabu vya CAG vinaandikwa kila mwaka hali inakuwa hivyo hivyo , lazima tuchukue hatua, uamuzi wa kuagiza serikali sina lakini uwezo wa kushauri ninao,”amesema Kinana.
Ameongeza kuwa bahati nzuri yeye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM na kazi zake ni mbili tu , mosi kukaa kwenye kiti cha mwenyekiti iwapo hayupo na kawaida mar azote mwenyekiti anakuwepo na kazi ya pili ni kumshauri mwenyekiti na kusema yale ambayo Mwenyekiti amemuagiza.
“Ukiona nasema basi Mwenyekiti mwenyekiti kanituma, hivyo hamtanishataki, hivyo nayosema nasema kwa niaba yake.Nawashauri waliohusika kwenye ripoti ya CAG hatua zichukuliwe, ili fedha za wananchi zisichezewe na wengi waliotajwa huko ndani wamekula kiapo cha uadilifu, hivyo natoa mwito huu kwa vyombo vya serikali.
“Nimeagiza kistaarabu tunatoa ushauri, hata hivyo kikao cha chama ndicho kinachoweza kutoa maagizo.Nashauri jambo hili lakini nina nafasi ya kumshauri Mwenyekiti wangu ili hili jambo likapate baraka ya vikao,”amesema.
Kinana amewataka watendaji na wafanyakazi kutosubiri maelekezo ya Rais.” Si kila jambo lazima Rais aagize.. tujenge utamaduni wa kuwajibika sisi wenyewe”