Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewaonya wanachama wa chama hicho kuacha kupanga safu katika nafasi mbalimbali za uchaguzi wa chama hicho ulioanza mapema mwezi huu.

Pia amesema chaguzi na nafasi ndani ya CCM hazina umiliki ndani ya chama hicho kwani hamna mwenye haki zaidi ya mwingine.

Aidha, ametoa wito kwa wanachama hao kujitokeza kutimiza haki yako ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa bila kubabaishwa, kutishwa wala kuogopeshwa na mazingira yoyote.

Chongolo ametoa kauli hiyo jana tarehe 10 Aprili, 2022 katika mkutano wa mapokezi ya Makamu mpya wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema viongozi wanaopanga safu na watu wanaowataka katika chaguzi mbalimbali hawana nia ya kutoa kiongozi bora atakayesukuma gurudumu la maendeleo mbele.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi, nimepewa jukumu la kuwa mkurugenzi mkuu wa uchaguzi kuanzia ngazi zote, toka tarehe 2 mwezi huu tulipiga kipenga uchaguzi wa mashina ndani ya wilaya zetu na waliochukua fomu ni wengi,” amesema.

Amesisitiza ni haki ya mwana CCM kujitokeza kutimiza haki yake ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.

“Jitokeze chukua fomu, usibabaishwe, usitishwe, usiogopeshwe, jipime, angalia mazingira, angalia uzito wako, zama nenda kachukue fomu,” amesema.

Amesema kuna tabia watu wanafikiria na kuanza kuota ubunge na udiwani wa mwaka 2025 ilihali muda bado.

“Tunao wabunge na madiwani chama hakina uhaba hadi 2025… wewe hangaika na uchaguzi huu wa ndani, acheni kupanga safu, acheni kutengeneza watu, sisi tunajua.

“Mwanasiasa mzuri ni yule anayehangaika na jambo kwa wakati mwafaka, hahangaiki na jambo la kesho,” amesema.

Amesema kwa kipindi kifupi alipoingia kwenye mkutano huo amepokea meseji zaidi ya 800 kutoka kwa watu mbalimbali wakiwafitini wagombea wenzao.