Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amefanya uhamisho na mabadiliko ya makamanda wa Polisi wa mikoa kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 6, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime imeeleza kuwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Onesmo Lyanga amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi, huku nafasi yake ikichukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Martin Otieno.

“Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Daniel Shillah amehamishwa kwenda kuwa kamanda wa polisi mkoa wa Kaskazini Unguja” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faustine Mafwele amehamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO).

“Aliyekuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (D/RCO) mkoa wa Mwanza Mrakibu Mwandamnizi wa Polisi (SSP) John Lwamlema anakuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO)” imeeleza taarifa hiyo