Na Janeth Mesomapya
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba amesema kuwa mafuta yaliyopo kwenye maghala, vituo vya mafuta pamoja na yale yanayoshushwa bandarini kwenye meli yanatosheleza mahitaji ya mafuta nchini.

Waziri Makamba ameyasema hayo Aprili 6, 2022 kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi ya Wizara jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwatoa hofu wananchi kufuatia ongezeko la bei za mafuta lililotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) jana.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja, watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara na Chama cha Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC).

“Hakuna uhaba wa mafuta nchini na hivyo hakuna haja kuwepo kwa taharuki juu ya malighafi hiyo. Mfumo wetu wa uagizaji na uingizaji mafuta ni mfumo thabiti ambao unatuhakikishia usalama wa mafuta nchini,” alieleza.

Waziri Makamba aliongeza kuwa hadi kufikia Aprili 1, 2022 petroli iliyokuwa kwenye maghala ni jumla ya lita 118,594,024 yanayotosheleza siku 27, dizeli lita 116,486,705 yanatosheleza siku 19, mafuta ya taa lita 6,823,710 yanatosheleza siku 108 na mafuta ya ndege lita 12,841,822 yanatosheleza siku 35.

Vilevile kuna meli ambazo zimewasili nchini na zinaendelea kushusha mafuta zikiwa na lita 86,256,000 za dizeli. Hivyo kwa kuzingatia mafuta yaliyokuwepo tarehe 01 Aprili 2022 nchi itakuwa na jumla ya lita 202,742,705 za mafuta ya dizeli zitakazotosheleza matumizi ya nchi kwa siku 33.

Pia kuna jumla ya lita 71,385,300 za petroli ambazo zipo katika meli zilizowasili nchini na hivyo nchi itakuwa na jumla ya lita 189,979,324 za mafuta ya petroli yakutosheleza siku 37.

“Kulingana na zabuni zilizokamilika, mafuta yataendelea kupokelewa hadi Juni 2022 na mafuta hayo yatatosheleza mahitaji ya nchi hadi mwisho wa Julai 2022. Vilevile, zabuni za kila mwezi zinaendelea kufanyika na zabuni inayofuata itakamilishwa mwishoni mwa mwezi huu” alibainisha.

Akilinganisha bei za mafuta katika soko la dunia kati ya Februari 2021 na Februari 2022, Waziri Makamba ameeleza petroli ilikuwa ni dola 561.74 kwa tani na kuongezeka dola 911.94, hii ni ongezeko la asilimia 62 huku dizeli ilikuwa dola 503.73 kwa tani na kuongezeka hadi dola 826.14 kwa tani ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 64.

Kwa upande wa mafuta ya taa bei ilikuwa ni dola 504.21 kwa tani ambayo ilipanda hadi kufikia dola 826.35 kwa tani ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 64.

Akielezea sababu za mfumuko huo wa bei za mafuta, Waziri Makamba amesema mgogoro wa kivita kati ya Urusi na Ukraine umepunguza uwepo wa mafuta katika soko la dunia baada ya NATO kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi ya Urusi ambayo inazalisha takribani asilimia 10 ya mafuta yanayozalishwa duniani.

“Upungufu huo wa mafuta umesababisha bei za mafuta katika soko la dunia kuongezeka kwa kiwango kikubwa kuanzia Februari 2022. Ifahamike kuwa, bei za mafuta zilianza kuongezeka Januari 2022 palipokuwa na tishio la kuwepo kwa vita na ongezeko la bei likawa kubwa zaidi vita ilipoanza,” aliongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC) Orlando Da Costa ameeleza kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini na bei iliyopo kwa sasa nchini ni nzuri ukilinganisha na nchi za jirani.