Serikali  imesema kuwa filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan, jijini New York, Marekani, itaitangaza Tanzania duniani, huku ikileta maelfu ya watalii kutoka nchini humo.

Katika uzinduzi huo uliofanyika katika jumba la Makumbusbo la Guggenheim 89th Avenue jijini New York, ulihudhuriwa na wadau wa utalii na watu mashuhuri wapatao 300, huku ikipambwa na burudani mbalimbali.

Filamu hiyo iliyochukua takribani saa moja imesheheni vivutio mbalimbali vya utalii, sanaa na burudani vinavyopatikana nchini Tanzania, vilivyotambulishwa kwa kuelezewa kwa kina na Rais Samia.

Akizungumzia filamu hiyo wakati wa mjadala wa viongozi wa serikali na taasisi zake uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbas, kipindi cha filamu ya saa moja inayotangaza utalii wa Tanzania kiliratibiwa na mtangazaji mashuhuri nchini Marekani, Peter Greenberg.

Alisema mwandishi huyo hushawishi viongozi wa nchi kuwa mbele kutangaza vivutio vya nchi yao na Tanzania ni nchi ya tisa duniani kushiriki mradi huo unaolenga kuitangaza nchi kwenye utalii ili ijulikane duniani.

“Kwa ujumla ni kui ‘repackage’ (kuviweka pamoja) nchi yetu ili ijulikane kote duniani, iwe ni sehemu ambayo watu wawe wanakuja siyo tu kutembea, kuona wanyamapori lakini pia kurekodi matukio makubwa ya kuburudisha,” alifafanua.

Dk. Abbas ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Royal Tanzania Tour, alisema ni mradi wa kwanza wenye kuhakikisha mazuri ya Tanzania yanafahamika ulimwenguni ikiwamo utalii, viwanda, sanaa na utamaduni.

Aliongeza kuwa filamu hiyo imezinduliwa Marekani kwa sababu lengo ni kuitangaza nchi kimataifa na kwa kuanzia wamealikwa watu washuhuri ikiwamo wafanyabiashara, wadau wa utalii na burudani.