Benny Mwaipaja, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa rai kwa wadau wa sekta ya mifugo nchini kuisadia serikali kutimiza nia yake ya kuimarisha uzalishaji wa nyama na maziwa ili kuongeza tija na kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo jijini Dodoma, alipokutana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki, wataalam kutoka Wizara hiyo na Wizara ya Fedha na Mipango, pamoja na Wazalishaji binafsi katika sekta za maziwa na nyama nchini.

Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa sekta ya mifugo itakuwa na mchango mkubwa katika kukuza kipato cha wananchi hususan vijana lakini pia itaongeza mapato ya nchi kwa kuzalisha bidhaa za nyama na maziwa zitakazo uzwa ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Aliwataka wadau hao kuwa walimu wa kuwaongoza na kuwafundisha vijana namna ya kuzalisha mifugo bora kwa ajili ya nyama na maziwa na kwa kuwa wana mtandao wa masoko, ni rahisi kwa wafugaji kupata maeneo ya kuuza mazao yao.

Dkt. Nchemba, alitoa wito pia kwa vijana na wawekezaji kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili wajipatie ajira katika sekta hizo muhimu badala ya kuwaachia wazee peke yao kujihusisha na masuala ya kilimo na mifugo na kuahidi kuwa Serikali iko tayari kuwawezesha maeneo na mitaji.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki, aliwahakikishia wadau hao wanaomiliki kampuni na viwanda vya kusindika nyama na maziwa kwamba Serikali iko tayari kushirikiana nao kuboresha sekta ya mifugo ili ilete tija nchini.

Aidha, alisema kuwa fedha zitakazoongezwa na Serikali katika Bajeti Kuu ya Mwaka 2022/2023 katika Wizara yake, zitaelekezwa kwenye maeneo yenye kuongeza uzalishaji ili kukuza ajira kwa vijana pamoja na kuzalisha mazao yatakayo kuza mauzo nje ya nchi.

Kwa upande wao, wadau wa Sekta ya mifugo walioshiriki kikao hicho, wameishauri Serikali kukuza sekta ya mifugo kwa kuwekeza kwenye masuala ya vipaumbele ikiwemo uhimilishaji, kuongeza huduma za ugani, afya ya mifugo na kujenga miundombinu ya kuchakata bidhaa za mifugo na kutafuta masoko ya uhakika.

Aidha, waliiomba Serikali kupitia upya masuala ya tozo na kodi kwenye sekta ya mifugo na kuzipunguza ili kuchochea uzalishaji wa sekta hiyo na pia kupunguza gharama za uzalishaji ambazo zitaifanya sekta hiyo kushindana katika soko na kutoa bei nzuri kwa wananchi.

Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amemwelekeza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kuongeza bajeti ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo, ili sekta hizo muhimu ziweze kuboreshwa na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.