Na Munir Shemweta na Magreth Lyimo, WANMM TANGA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makakzi Dkt Angeline Mbuala ametaka elimu na ushirikishwaji wananchi kupewa kipaumbele wakati wa utekeleza maamuzi ya Baraza la Mawiziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975

Dkt Mabula alisema hayo mkoani Tanga tarehe 02 April 20202 wakati yeye na timu yake ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakitoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwa viongozi wa mkoa na wilaya katika mkoa huo kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi.

Katika maamuzi yake, Baraza la Mawaziri lilipendekeza vijiji 14 katika mkoa wa Tanga kubaki maeneo ya hifadhi na kufanyiwa marejebisho ya mipaka huku vijiji viwili na mitaa miwili kufanyiwa tathmni kutokana na sehemu kubwa ya maeneo yake kuwa na umuhimu kwa maslahi ya Taifa.

Katika mkoa wa Tanga maeneo yenye mgogoro wa matumizi ya ardhi yanahusisha wananchi na Hifadhi ya Msitu wa Mikoko na Shamba la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo katika Kituo cha TALIRI,

Maeneo mengine ni kwenye Hifadhi za Misitu Chang’andu, Kwani na Gendagenda pamoja na mgogoro katika Pori Tengefu la Mto Umba na ule wa Shamba la Mwele-ASA.

‘’Rai yangu katika utekelezaji maamuzi haya ya Baraza la Mawaziri ni ushirikishwaji ili asitokee mtu akalalamika kaonewa au kafanyaje, jukumu letu kama serikali  ni kuhakikisha tunatoa elimu pia ili masuala haya yasijirudie kwa sababu tumekuwa na operesheni mbalimbali ambazo mwisho wa siku utekelezaji au usimamizi wake ubakuwa siyo mzuri sana’’

‘’Kipindi hiki Mhe mama Samia asingependa kuona masuala haya ya migogoro ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali yanajirudia ndiyo maana katika Wizara ya Ardhi ametoa fedha nyingi ili kumalizana na migogoro ya ardhi’’.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alisisitiza suala la uwajibikaji kwa watendaji wa serikali kuanzia mkoa hadi kijiji na kuwataka kila mmoja kusimamia majukumu yake ili masuala ya uvamizi kwenye hifadhi na taasisi za umma yasijirudie.

‘’Tunaporekebisha maeneo haya hatutarajii tena uvunjifu wa sheria uendelee uongozi kuanzia ngazi ya kijiji muwe walinzi wazuri wa maeneo hayo ili kuepuka migogoro hiyo ya wananchi kujimegea maeneo ambayo siyo rasmi kwa makazi’’ alisema Dkt Mabula.

Mawaziri walioko kwenye ziara hiyo mkoani Tanga walielezea hatua na mikakati ya kuchukua wakati wa utekelezaji Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa Migogoro katika vijiji 975.

Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo Abdallah Ulega alisisitiza suala la watendaji wa serikali kuwa imara wakati wa kusimamia zoezi zima la utekelezaji maamuzi hayo ili kuepuka kupata tabu kwenye utekelezaji.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Hamis Chillo aliwahimiza watendaji wa serikali kuhakikisha wanasimamia na kutunza mazingira hususan kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kusisitiza utumiaji busara wakati wa utekelezaji maamuzi ya baraza la Mawaziri.

Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo alielezea mikakati ya serikali kupitia wizara yake katika kujikita kwenye uzalishaji mbegu ili kukidhi mahitaji ya nchi na kuepuka uagizaji mbegu kutoka nje ya nchi sambamba na kufanya  utafiti katika mashamba yake yaliyovamiwa.

Waziri wa Ardhi Dkt Mabula ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Kisekta aliwaasa wananchi hasa waliotengewa maeneo yaliyowekewa mipango ya matumizi ya ardhi kuwa, serikali haitarajii kuona tena wakiingia maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji yaliyozuiliwa kwa kuwa uvamizi uliofanywa ndiyo uliosababisha migogoro ya matumizi ya ardhi.

‘Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Wizara yake  isingependa kuona mambo haya yanajirudia na  wale wote ambao mara nyingi wanavamia maeneo na kutarajia serikali kuridhia kuendelea wawepo  maeneo hayo, suala hili  halitajirudia tena na kinachotakiwa sasa kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa kutii sheria bila shuruti kwani serikali haiwezi  kuwa na mazoezi haya kila mwaka.