Akaunti ya YouTube ya msanii Diamond Platnumz imerejea baada ya kuripotiwa kuchukuliwa na wadukuzi jambo ambalo lilisababisha kufungwa kwa akaunti hiyo.

Chaneli ya Diamond Platnumz, ambayo ina watumiaji zaidi ya milioni 6.5 na yenye kutazamwa na watu zaidi ya bilioni moja, ilisemekana kuwa ilidukuliwa siku ya Jumapili.

Ofisa wa kampuni ya rekodi ya Diamond Platnumz, Wasafi, alisema kuwa walipokea barua pepe kutoka YouTube ikiwajulisha kuwa akaunti hiyo imesimamishwa.

Majid Ramadhani alisema ilisitishwa baada ya wadukuzi hao kuweka wazi maudhui ambayo yalikiuka miongozo ya jukwaa la kidigitali.
 

Siku ya Jumatatu, nyota huyo wa muziki aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram akionyesha kuwa ukurasa huo umerejea.