Benny Mwaipaja, Washington DC
BENKI ya Standard Chattered imeihakikishia Tanzania kuwa iko tayari kutoa fedha zaidi kwenye miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ikiwemo Reli ya kisasa ya SGR na ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege.

Ahadi hiyo imetolewa na Uongozi wa Benki hiyo ukjongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Jose Vinals, ulipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb). kando ya mikutano ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Jijini Washington DC, Marekani.

Akizungumza baada ya kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, Washington DC, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba alisema kuwa Benki hiyo ilitoa mkopo unaotumika kujenga reli ya kisasa ya SGR kutoka Morogoro hadi Makutupora, mkoani Singida, na kwamba hivi sasa Serikali iko kwenye mazungumzo na Benki hiyo ili itoe mkopo mwingine kwa ajili ya vipande vingine vya reli hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, alisema kuwa katika kuimarisha shughuli za utalii na kukuza uchumi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepanga kuboresha miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Pemba na kwamba mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali na Benki hiyo yatawezesha kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Standard Chartered baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Benki hiyo nchini Tanzania Bw. Sanjay Rughani, alisema kuwa wako tayari kutoa fedha zaidi kwa ajili ya miradi iliyowasilishwa na Serikali kwenye Benki hiyo.

Alisema kuwa pamoja na ahadi ya kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, Benki hiyo pia iko tayari kuwashawishi wawekezaji wengine kutoka maeneo mbalimbali duniani kwenda kuwekeza mitaji na teknolojia nchini Tanzania.

Ikumbukwe kwamba Benki ya Standard Chartered, tarehe 13 Februari, 2020, iliipatia Tanzania mkopo wenye thamani ya dola za Marekani, bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kipande cha kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Singida