SERIKALI imesema kuwa pamoja na mwenendo mzuri wa ukuaji wa Uchumi nchini vipo viashiria vingine vya Uchumi ambavyo vimekua na matokeo mazuri zaidi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha taarifa yake ya mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Dk Nchemba amesema ukwasi au mzunguko wa fedha katika Uchumi uliongezeka kwa wastani wa asilimia 9.3 katika kipindi cha mwaka unaoisha Desemba 2021 ukilinganisha na asilimia 4.8 Desemba 2020.
Amesema ukuaji huo unatokana na kuongezeka kwa mikopo katika sekta binafsi na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuhakiki na kulipa malimbikizo ya madeni mbalimbali yakiwemo ya watumishi, wazabuni na wakandarasi.
Amesema mikopo katika sekta binafsi iliongezeka kufikia ukuaji wa asilimia 10 Desemba 2021 ikilinganishwa na asilimia 3.1 Desemba 2020 kutokana na kufunguka kwa fursa mbalimbali katika shughuli za kiuchumi.
Dk Nchemba amesema Serikali ya awamu ya sita imepunguza mikopo kichefuchefu katika sekta ya benki ambayo ilipungua hadi asilimia 8.2 Desemba 2021 ikilinganishwa na asilimia 9.3 ya 2020.
" Akiba ya fedha za kigeni iliongezeka hadi Dola za Marekani Bilioni 6.4 Desemba ikilinganishwa na Dola Bilioni 6 mwaka 2020, Kiasi hiki kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka Nje ya nchi Kwa kipindi kisichopungua miezi sita na ni ziada ya lengo la Nchi za Afrika Mashariki na miezi minne hadi sita kwa Nchi za SADC.
Kuhusu mfumuko wa bei, Dk Nchemba amesema kipindi chote cha awamu ya sita mfumuko umeendelea kubaki chini ya asilimia tano kama ilivyopangwa katika malengo ya muda wa kati na katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
" Mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 4 kwa mwaka 2021 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.7 mwaka 2020, Aidha mfumuko wa bei umeshuka na kufikia asilimia 3.7 Februari 2022 ikilinganishwa na asilimia 4 ya Januari 2022 na hii ni kutokana na utekelezaji mzuri wa sera za fedha na Bajeti,.
Eneo la mapato kati ya Julai 2021 hadi Februari 2022 mapato ya ndani yameongezeka hadi Sh Trilioni 15.9 sawa na asilimia 93.5 ya makadirio ya kipindi hicho ya kukusanya Sh Trilioni 17," Amesema Dk Nchemba.
Amesema kati ya Julai 2021 hadi Februari 2022 Serikali imepokea jumla ya Sh Trilioni 3.1 kutoka kwa washirika wa maendeleo kama misaada na mikopo nafuu sawa na ufanisi wa asilimia 119.2 ya matarajio ya kupokea Sh Trilioni 2.6 ikilinganishwa na Sh Trilioni 1.6 iliyopokelewa mwaka 2020 hadi 2021.