Na Waandishi wetu, Dar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea nakala ya Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Malawi nchini Mhe. Andrew Kumwenda leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam

Baada ya kupokea nakala ya hati hizo Balozi Mulamula amemuahidi Balozi mteule ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi wakati wote atakaokuwepo nchini.

“Leo nimepokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Malawi na tumefarijika kwa Mhe. Rais Chakwera kumteua Balozi huyu mara baada ya Balozi wa awali kumaliza muda wake wa uwakilishi, hii ni ishara ya uhusiano wa karibu, undugu na urafiki uliopo baina ya Tanzania na Malawi,” amesema Balozi Mulamula

Kwa upande wake Balozi Mteule wa Malawi Mhe. Andrew Kumwenda amesema kuwa Malawi na Tanzania siku zote zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na jukumu langu hapa kama Balozi ni kuhakikisha uhusiano huu unazidi kuku ana kuimarika.

“Tanzania inatekeleza Diplomasia ya Uchumi na vivyo hivyo Malawi………kwa hiyo sisi wote tuna lengo moja, na nitahakikisha Tanzania na Malawi zinashirikiana kufanya biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande mbili,” Amesema Balozi Kumwenda.