Na WMJJWM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima Tanzania inaendelea kuwezesha wanawake kumiliki ardhi  na kuushiriki kwenye mipango ya matumizi ya ardhi iliyopo vijijini na utoaji wa maaamuzi katika changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akishiriki katika Mkutano wa pembeni ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.

Dkt. Gwajima amesema kuwa Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mwanamke anapata fursa ya kumiliki ardhi hasa kwa wanawake wanaoishi vijijini kwani kumekuwa na changamoto katika kumiliki na kushirikishwa katika maamuzi ya matumizi ya ardhi hasa katika kilimo.

“Katika hili tumeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha Mwanamke na Mtoto wa Kike anawezeshwa kumiliki ardhi na kushiriki katika kuamua matumizi bora ya ardhi na kunufaika nayo” alisema Waziri Dkt. Gwajima

Waziri Dkt. Gwajima ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Amon Mpanju sambamba na Wataalam wa Wizara amesema, Mkutano wa Hali ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2022 unaongozwa na kauli mbiu ya “Kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na watoto wa kike kwa kupitia programu na sera yenye mtazamo wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira na upunguzaji wa athari za majanga”

Wakati huo huo wataalam wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Idara ya Maendeleo ya Jinsia kwa kushirikiana na wadau wameshiriki Mkutano huo kwa njia ya Mtandao wakiwa  Jijini Dodoma ikiwa ni kuupa nguvu Mkutano unaoendelea nchini Marekani na kutia msukumo ajenda iliyojadiliwa katika mkutano huo.

Akizungumza baada ya Mkutano huo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara ya Maendeleo ya Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Rennie Gondwe amesema lengo la Mkutano huo wapembeni ndani ya Mkutano wa 66 wa hali ya Wanawake Duniani ni kuhamsisha jamii na kuwa na usawa na haki katika kumiliki na kutumia ardhi na kutoa maamuzi.

Rennie amesema kuwa, Wizara kwa kushirikiana na wadau inatekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wenye maeneo manane ikiwemo eneo la Mila na Desturi ambapo unasaidia pia kutoa hamasa kwa jamii na wadau kutoa elimu ya kumuwezesha Mtoto wa kike na Mwanamke kumiliki na kunufaika na ardhi.

Akichangia kwenye Mkutano huo Mkurugenzi wa Landesa Tanzania Dkt. Monica Mhoja, amesema Shirika lake linashirikana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha mwanamke haachwi nyuma kunapo umiliki wa ardhi na kupata manufaa  hasa katika uzalishalishaji na matumizi bora ya ardhi.

Ameongeza kuwa lengo la Shirika hilo ni kuangalia ni kwa namna gani makundi hasa ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashirikishwa kwenye mpango wa matumizi ya ardhi hususan katika ngazi ya kaya ili ardhi hiyo iweze kuwanufaisha katika ustawi wao.