Watu watano wa familia moja wanadaiwa kufariki dunia baada ya kupigwa na radi katika Kijiji cha Kamsisi Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani humo Ali Makame Hamad amesema watu hao ni Masalu Sengule (32) Muri Shija (25) Nkiya Masalu (7) Vumi Masalu (5) Mariam Masalu (miezi mitano) ambao ni familia mojana  wote ni wakazi wa Kijiji hicho.

Kamanda Hamad amesema tukio hilo limetokea Machi 2, 2022 ambapo mvua kubwa ilinyesha iliyoambatana na radi na kuwapiga wakiwa wamelala usiku.

Pia ameongeza kuwa mbali na watu hao watano, watu wawili wamepoteza maisha katika tukio jingine la kupigwa na radi huko Kijiji cha Mlibanzi kilichopo wilaya ya Tanganyika Mkoani humo.

Kwa mujibu wa Kamanda Hamad amesema watu hao ambao ni Faines Mihani (37) na Elizabet Nyandwi (13) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Mlibanzi walikutwa na mauti hayo wakiwa shambani wanalima.

Miili ya marehemu wote saba imeshafanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.