Ofisi ya Bunge inawajulisha Wabunge wote kufika Dodoma siku ya Alhamisi tarehe 10 Machi, 2022 kwa ajili ya Shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Bunge wa Bajeti.
Watakapofika Dodoma watashiriki Mkutano wa Wabunge wote utakaofanyika siku ya Ijumaa tarehe 11 Machi, 2022. Katika mkutano huo, Waziri wa Fedha atawasilisha kwa Wabunge Mapendekezo ya Serikali ya Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni 2020.
Baada ya Mkutano huo, Kamati zitaendelea na shughuli zilizopangwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kama ifuatavyo:-
(i) Kamati Tisa za Kisekta zitatembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 kwa mujibu wa Kanuni ya 117 (1) ya Kanuni za Bunge.
(ii) Kamati ya Bajeti itachambua Mapendekezo ya Serikali ya Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (4) ya Kanuni za Bunge.
(iii) Kamati za Kisekta zitafanya vikao vya kuchambua taarifa za utekelezaji wa bajeti za Wizara zinazozisimamia kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 na kufanya ulinganisho na makadirio ya matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 kwa mujibu wa Kanuni ya 117 (2) ya Kanuni za Bunge.
(iv) Kamati ya Uongozi pamoja na Kamati ya Bunge ya Bajeti zitafanya kikao cha mashauriano kuhusu mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye Kamati za Kisekta wakati wa kujadili utekelezaji wa bajeti za Wizara mbalimbali na Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa mujibu wa Kanuni ya 117 (4) ya Kanuni za Bunge.
(v) Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo itapokea taarifa za utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na kuchambua Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Sita wa Bunge.
(vi) Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitafanya ziara za ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
(vii) Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya ziara ya ufuatiliaji wa ufanisi na tija ya uwekezaji wa mitaji ya umma kwenye miradi mbalimbali ya kiuwekezaji.
Ratiba ya Shughuli za Kamati za Bunge inapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.bunge.go.tz.
Imetolewa na:- Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge
Mtaa wa Makole
411480 DODOMA