Serikali imewataka viongozi wa dini nchini kuwaelimisha waumini wake umuhimu wa kuhesabiwa katka sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha, imewataka viongozi wa dini kuendelea kusaidia katika suala zima la malezi ya kiroho ili kujenga jamii yenye kumcha mungu, uadilifu na ubinadamu.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa Kutabaruku Kanisa la Bikira Maria wa Fatima Geita mwishoni mwa wiki, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi ambazo bila ya kuwa na takwimu sahihi haitaweza kupanga mipango thabiti ya matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

‘’Viongozi wa Dini mnao waumini wengi tumieni fursa hiyo kuwaelimisha waumini wenu umuhimu wa kuhesabiwa’’ ilieleza hotuba ya Waziri Mkuu.

Alisema, zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa kuwa linaipatia nchi takwimu za msingi zinazotumika kutunga sera, kupanga mipango na program za maendeleo pamoja na kufuatilia utekelezaji wake.

Kupitia hotuba hiyo, Dkt Mabula alieleza kuwa, takwimu rasmi zitawezesha serikali na wadau wenghine kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika kutekeleza mipango ya maendeleo iliyokusudiwa sambamba na chanagmoto mbalimbali zitakazojitokeza katika sekta zote na hatimaye kuweka malengo na mikakati ya kukuza uchumi pamoja na kupunguza umasikini miongoni mwa watanzania.

Aidha, ilieleza kuwa, hivi karibuni kumekuwa matukio yanayohusisha mauaji ya raia kwa raia , moto kwenye masoko na baadhi ya raia kujinyonga ambapo alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kulitaka jeshi la polisi kuweka mikakati ya kuhakikisha jamii inatoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vya kihalifu.

‘’Niwaombe viongozi wetu wa taasisi za dini kuendelea kusaidia katika suala zima la malezi ya kiroho ili kujenga jamii yenye kumcha mungu , uadiliufu na ubinadamu’’ ilieleza hotuba ya Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Baba Askofu Flavian Kasala ambaye ni Padre wa kwanza wa Parokia hiyo ya Bikira Maria wa Fatima tangu kuanzishwa kwake alisema, viongozi wa dni wataendelea kuiunga mkono serikali katika suala zima la sensa ya watu na Makazi kwa kuwa suala hilo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

‘’Sisi tutaendelea kuinga mkono serikali na uwepo tofauti ndogo ndogo ndizo zimewapeleka baadhi ya watu kwenye matatizo makubwa na tusiruhusu jambo hilo linaloweza kututofautisha kwenye imani zetu za kidini’’ alisema Askofu Flavian Kasala

Hafla ya kubariki Kanisa la Bikira Maria wa Fatima Jimbo la Geita ambalo ujenzi wake ulianza Januari 03, 2020 na kukamilika Machi 18, 2022 na kugharimu takriban Bilioni 1.9 iligawanyika sehemu ya kutabaruku Kanisa kwa kunyunyizia maji ya Baraka nje na ndani ya kanisa, kupaka mafuta ya krisma altare mpya pamoja na nguzo 12 na kuendelea na ibada ya misa takatifu iliyoanza saa tatu asubuhi hadi saa kumi jioni.

Aidha, kupitia hafla hiyo Dkt Angeline Mabula aliongoza harambee kwa ajili ya kuchangia ukamilishaji Samani za Kanisa ambapo kiasi cha shilingi 88,725,000/- kilipatikana kwa fedha taslim na ahadi kutoka kwa watu mbalimbali.

‘’Uwepo wa jengo hili jipya, kubwa na zuri la Kanisa la Bikira Maria wa Fatima ni ushuhuda wa kukua kwa imani ya kanisa kwa waumini wake ambapo sasa ni miaka 65 imepita tangu injili ilipoingia ukanda huu wa Altare ya kwanza ya Jimbo la Geita ilikuwa katika uwanja lililopojengwa jengo hili jipya’’ alisema Askofu Kasala