WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameliomba Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani – USAID, kuelekeza kiasi cha msaada wa dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3 inazotaka kuipatia Tanzania kupitia Asasi za kiraia, katika kipindi cha miaka 5 ijayo, zielekezwe kwenye miradi ya kipaumbele ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Dkt. Nchemba ametoa maombi hayo Mjini Dodoma, alipofanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bi Kate Samvongsiri.
Alilishukuru Shirika hilo kwa uamuzi wake wa kutoa kiasi hicho cha fedha kupitia Asasi za Kiraia (NGOs) katika kipindi cha miaka mitano ijayo lakini akaeleza umuhimu wa miradi iliyokusudiwa kutekelezwa na asasi hizo za kiraia kuelekezwa katika vipaumbele vya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo sekta za afya, elimu, kilimo, na mingineyo itakayochochea ukuaji wa uchumi.
“Tunapoandaa ushirikiano mpya na mipango mipya tunaomba mzingatie vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambayo amewekeza nguvu kubwa, sambamba na yale mnayofanya kwenye sekta ya afya, elimu, kilimo, mazingira, pamoja na sekta zingine”Alisema Dkt. Mwigulu
Dkt. Mwigulu alisema kwa sasa Mhe Rais anajenga vituo vingi vya afya na hivi karibuni ataajiri watumishi wengi wa sekta hiyo, pamoja na sekta zingine ambazo anazifanyia kazi kama sekta ya elimu na kuiomba USAID kuelekeza fedha hizo ambazo nitapitia kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kwenye maeneo hayo.
“Mfano, vituo vya afya vingi vimejengwa na watumishi wataajiriwa, mnaweza mkaweka nguvu kwenye vitendea kazi ambavyo bado havijakamilika ili huduma ziwe zinapatikana na lengo la Serikali pamoja na malengo mliyonayo ya kuendeleza huduma za jamii ambalo mnalo liweze kutimia” Alisema Mwigulu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani -USAID, Bi Kate Samvongsiri, alisema kuwa wanapenda kushirikiana na Serikali ya Tanzania na watakaa pamoja na kuangalia shughuli zinazofanyika katika sekta hizo za elimu, afya, kilimo, maji pamoja na zingine na kuona namna watakavyoziwezesha.
Uhusiano kati ya Tanzania na Shirika hilo la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID, limekuwa na uhusiano wa zaidi ya miaka 50, na kwamba tarehe 30 Septemba, 2016, Shirika hilo lilisaini mikataba mitatu ya msaada yenye thamani za zaidi ya dola za Marekani milioni 635.5, zilizotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, program ambayo itafikia tamati mwezi Septemba, 2022