Na. Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha

Kamanda wa Polisi MKoa wa Arusha ACP JUSTINE MASEJO amesema kuwa Tarehe 09.03.2022 muda wa saa 07:00 mchana huko eneo la mto Ngarusi kijiji na kata ya Alaitore, tarafa ya Ngorongoro, wilaya ya Ngorongoro na Mkoa wa Arusha NARUDWASHA TITIKA (45) mfugaji mkazi wa kijiji cha Alaitore kilichopo ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro alifariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya tembo sehemu mbalimbali za mwili wake.

ACP Masejo amesema Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa marehemu alikutwa na mkasa huo wakati akitafuta kuni akiwa na wenzake ndani ya hifadhi ndipo alipo shambuliwa na tembo huyo. Aidha mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi baada ya uchunguzi wa daktari.

Ameendelea kusema Kamanda Masejo kuwa katika tukio jingine ni kwamba tarehe 09.03.2022 muda wa 04:00 asubuhi huko katika kitongoji cha Karafia kijiji cha Kisimiri wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha askari wakiwa katika operesheni walifanikiwa kuharibu shamba lenye ukubwa wa ekari tano (05) likiwa na miche idhaniwayo kuwa madawa ya kulevya aina ya bhangi.

Ameeleza kuwa mtuhumiwa wa shamba hilo aliyefahamiwa kwa jina moja la Babu alitumia mbinu ya kuchanganya miche hiyo ya bhangi pamoja na mazao aina ya mahindi.

Amewaambia kuwa Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kumtafuta mmiliki wa shamba hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi wanaoishi katika hifadhi kuchukua tahadhari katika maeneo ya hifadhi za wanyama pori na kuhakikisha wanafuata maelekezo mbalimbali yanayotolewa na mamlaka za uhifadhi, Pia nitoe wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi hususani kwa kuwatumia askari kata kuhusiana na baadhi ya watu wanao jihusisha na kilimo cha madawa ya kulevya pamoja na uuzwaji wa madawa hayo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.