Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetakiwa kujikita katika kukuza mapato ya ndani ili kuweza kuboresha huduma zake za msingi.

Hayo yalizungumzwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Seleman Kakoso (MB) katika semina ya kujenga uelewa wa majukumu na huduma zitolewazo na TMA, iliyofanyika katika Ukumbi wa TMDA, Mwanza, Tarehe 15/03/2022.
 
Mhe. Kakoso aliitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kujikita katika kukuza mapato ya ndani ili kuweza kuboresha huduma za kimsingi za hali ya hewa na hivyo kufikia malengo.
 
Aidha, Mhe. Kakoso aliendelea kwa kusisitiza kuwa ili kuwa na utabiri wa uhakika wa hali ya hewa, Mamlaka inahitaji vitendea kazi vya kutosha ambavyo upatikanaji wake unahitaji fedha za kutosha kutoka serikalini, na hivyo, kuitaka TMA kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira kwa kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta ya mazingira kwa lengo hilohilo la kuongeza mapato. Mhe. Kakoso alimalizia kwa kuipongeza TMA kwa kutoa huduma bora za hali ya hewa hapa nchini.
 
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) alimpongeza Mkurugenzi Mkuu na watumishi wa TMA kwa kazi nzuri inayofanyika na kuwaasa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kutembelea Ofisi za TMA ili waweze kujionea kwa kina majukumu na huduma mbali mbali zitolewazo.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru Kamati ya Bunge kwa fursa iliyopatikana ya kutoa elimu ya mchango wa huduma za hali ya hewa katika kukuza uchumi wa nchi.
Vilevile alieleza kuwa majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambayo ni kutoa huduma za hali ya hewa, kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha kumi na nne (14) na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini kulingana na Kifungu cha tano (5) cha Sheria yaMamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya Mwaka 2019.
 
Katika hatua nyingine, wajumbe walipata fursa ya kutembelea rada ya hali ya hewa iliyopo Kiseke, Mwanza na kupitishwa katika mada mbalimbali za kuwajengea uelewa juu ya majukumu na mchango wa huduma za hali ya hewa zitolewazo na TMA kwa manufaa ya jamii na kuchangia katika kukuza uchumi kupitia matumizi ya huduma hizi katika sekta mbalimbali nchini.
 

Wajumbe waliipongeza Mamlaka kwa kazi nzuri na kuelekeza TMA ihakikishe huduma za hali ya hewa zinawafikia wakulima katika ngazi ya vijiji.