Tanzania Yashiriki Makabidhiano Ya Majukumu Ya Baraza La Amani Na Usalama La Umoja Wa Afrika
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shiyo ameongoza ujumbe wa Tanzania katika hafla ya kupokea majukumu ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yaliyokabidhiwa kwa Nchi 15 wanachama wapya, Tanzania ikiwemo na wajumbe wa Baraza hilo wanaomaliza muda wao.
Hafla hiyo ambayo imefanyika hivi karibuni jijini Maseru, Lesotho na kuratibiwa na Sekretarieti ya Umoja wa Afrika, ilitanguliwa na warsha iliyolenga kuwawezesha Wajumbe wa Baraza kubadilishana uzoefu na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya Baraza hilo.
Wakati wa warsha hiyo ambayo ilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa wa Ufalme wa Lesotho, Mhe. Mats’epo Ramakoae, Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi Wanachama 15 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika walibadilishana uzoefu kuhusu mamlaka na taratibu za Baraza hilo, vihatarishi kwa amani na usalama barani Afrika na namna ya kuimarisha ufanisi wa Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Afrika. Aidha, maeneo ambayo yanakusudiwa kupewa kipaumbele na Baraza jipya pia yalijadiliwa.
Akizungumza baada ya warsha hiyo, Mhe. Balozi Shiyo alieleza kuwa, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika na watu wa Afrika kwa ujumla wana matarajio makubwa kwa chombo hicho katika kuchangia na kuimarisha hali ya amani na usalama barani Afrika, Bara ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi. “Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa mchango wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutumia Baraza la Amani na Usalama kutatua changamoto za kiusalama na kuimarisha amani na utulivu barani Afrika” alisema Balozi Shiyo.
Itakumbukwa kuwa,Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2022. Tanzania itahudumu kwenye Baraza la Amani na Usalama kwa kipindi cha miaka 2 kuanzia tarehe 01 Aprili 2022. Nchi 15 Wanachama wapya wa Baraza jipya la Amani na Usalama ni Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Gambia, Ghana, Morocco, Namibia, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa Mkataba ulioanzisha Umoja wa Afrika, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ni chombo cha kudumu na cha maamuzi kuhusu masuala yote yanayohusu kuzuia, kukabiliana na kusuluhisha migogoro barani Afrika.