Tanzania na Ireland zimeahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo kwa manuufaa ya pande zote mbili

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa ahadi hiyo aliposhiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mtakatifu Patrick ambayo huadhimishwa na Jamhuri ya Ireland tarehe 17 ya kila mwaka.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku hiyo Waziri wa Mulamula ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Ireland kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania hasa katika Nyanja za kusaidia kaya masikini, elimu na kuwajengea uwezo wanawake na watoto wa kike nchini.

Amesema Serikali inathamini mchango wa Ireland kwa Tanzania na kusisitiza kuwa itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo ili kufikia maendeleo ya kweli kwa pamoja.

Naye Balozi wa Ireland nchini Mhe. Mary O’Neil ameahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada za kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Ireland na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa faida ya wananchi wa nchi zote.

Maadhimisho ya siku hiyo yamezinduliwa rasmi leo Tarehe 02 Machi 2022 jijini Dar es Salaam katika makazi ya Balozi wa Ireland nchini na kuhudhuriwa na Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa wanaoziwakilisha nchi na Mashirika yao hapa nchini.

Siku ya Mtakatifu Patrick huadhimishwa kila ifikapo tarehe 17 Machi nchini Ireland kuadhimisha kuwasili kwa ukristo nchini humo na kusherehekea urithi wa utamaduni wa watu wa Ireland kwa ujumla.