Na. Veronica E. Mwafisi-Dar-es-Salaam
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa kielektroniki wa kupokea, kufuatilia na kushughulikia malalamiko (e-Mrejesho) kumekuwa na mwitikio chanya wa wananchi na watumishi wa umma kuutumia mfumo huo, ambao umeiwezesha Serikali kupokea na kushughulikia kwa wakati jumla ya maoni na malalamiko 239,196 yaliyowasilishwa katika Taasisi za Umma.
 
Bw. Daudi amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya matumizi na uendeshaji wa mfumo wa kutuma, kupokea na kufuatilia malalamiko, mapendekezo, maulizo na pongezi (e-Mrejesho) kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA wa Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara, Wakala na Idara Zinazojitegemea ambao wamepewa dhamana ya kushughulikia malalamiko kwenye taasisi zilizopo Kanda ya Mashariki.
 
Bw. Daudi amesema kuwa, miaka ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo wa kielektroniki haikuwa rahisi kushughulikia malalamiko kwa wakati na kuwa na takwimu halisi za maoni na malalamiko yaliyofanyiwa kazi ambazo zinatumiwa na Serikali kama mrejesho wa kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma kwa wananchi.
 
Aidha, Bw. Daudi ameeleza kuwa, Ofisi ya Rais – UTUMISHI kupitia Idara ya Ukuzaji Maadili imejipanga kuendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA katika taasisi zote za umma nchini, ili kuwajengea uwezo wa kutumia vema mfumo huo wa kieletroniki kushughulikia malalamiko yote yanayowasilishwa na wananchi na wadau kwa wakati.
 
Bw. Daudi ameongeza kuwa, Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa kwa namna ambayo inaongeza uwazi, uwajibikaji na usikivu kwa watendaji Serikalini, kwani mfumo unawawezesha viongozi katika ngazi mbalimbali kuona na kufuatilia namna ambavyo malalamiko au maoni yanavyoshughulikiwa.
 
“Endapo kutakuwa na ucheleweshwaji wa kutoa mrejesho au uzembe wa aina yoyote, mfumo unampa fursa kiongozi katika taasisi husika kuchukua hatua stahiki kwa wakati,” Bw. Daudi amefafanua.
 
Sanjari na hilo, Bw. Daudi amesema kuwa, mfumo huo ni rahisi kuutumia kwa kuwa unamuwezesha mtumishi na mwananchi wakati wote na popote alipo kutuma maoni au malalamiko na kupokea mrejesho kupitia tovuti au simu za kiganjani.
 
Akisisitiza suala la uwajibikaji, Bw. Daudi ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo, kuhakikisha wanaratibu ushughulikiaji wa malalamiko kwa wakati ili mfumo huo uwe na tija kwa wananchi na manufaa kwa Serikali katika kuboresha huduma inazozitoa kwa wananchi.
 
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu kuzungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Bi. Leila Mavika amesema kuwa, njia ambazo zilikuwa zikitumika kuwasilisha malalamiko hapo awali zilisababisha changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosekana kwa takwimu sahihi za utunzaji wa takwimu za malalamiko ambazo hutumiwa na Serikali kuboresha huduma na kufanya maamuzi.
 
Bi. Mavika ameeleza kuwa, kabla ya Serikali kuanzisha mfumo wa kushughulikia malalamiko kielektroniki, wananchi hawakuwa na fursa ya kupata mrejesho wa malalamiko yao kwa wakati hivyo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) iliona ni vema kuandaa mfumo wa kielektroniki ambao kwa kiasi kikubwa utaongeza uwajibikaji katika eneo la kushughulikia malalamiko.
 
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara yake ya Ukuzaji wa Maadili na Idara ya Mifumo ya TEHAMA inatoa mafunzo ya kutumia mfumo wa e-Mrejesho kwa Maafisa Malalamiko na TEHAMA katika Taasisi za Umma ziliozopo mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, yanayofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku nne (4) katika Ukumbi wa Chuo cha Kodi.