Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuchukua hatua za mapema ili kuepuka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.

Aliyasema hayo alipokuwa akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa nyumba 644 za wakazi wa Magomeni, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni – Dar es Salaam, Tarehe 23 Machi 2022.

“ Niwakumbushe leo ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani, niwaombe wananchi wote kufuatilia taarifa za hali ya hewa. Huu ni mwezi wa tatu na mwezi wa nne tunategemea Masika na mvua zimeanza kuonesha makali yake, kwa hiyo niwaombe sana mfuatilie taarifa za hali ya hewa ili kujiepusha na majanga mapema, mtakapopata taarifa za hali ya hewa na tukazifuata, basi tutaepukana na majanga au maafa mapema ” Alisisitiza Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB) ametoa wito kwa watumiaji na wadau wote wa taarifa za hali ya hewa hususani kwa jamii inayoathirika zaidi na maafa yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa, kufuatilia taarifa na kuchukua tahadhari pamoja na kuwataka kuunga mkono mipango ya Serikali katika uboreshaji wa huduma hizo.

Aliyazungumza hayo alipozungumza na vyombo vya habari katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani-2022 yenye kauli mbiu “Tahadhari kwa Hatua za Mapema” katika Ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka ya Bandari, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Mbarawa aliongeza kuwa, katika kuboresha huduma za hali ya hewa, Serikali ilitunga sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Na. 2 ya mwaka 2019 na inaendelea kuboresha miundombinu ya upimaji wa hali ya hewa kwa kununua RADA za hali ya hewa na vifaa vya kisasa na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa. Uwekezaji huu umechangia kuongezeka kwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kufikia kati ya asilimia 93 na 96, viwango ambavyo ni vya juu ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 70 kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuwa kinafaa kwa matumizi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alipata wasaa wa kuzungumza na wanahabari kwa kuelezea sababu zilizopelekea kuchaguliwa kwa kaulimbiu hiyo kuwa ni kutokana na ongezeko la maafa yanayotokana na hali mbaya ya hewa kwa wingi na kwa ukubwa wake hasa kwa kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi duniani.

Pia alisema endapo taarifa zikitolewa na tahadhari zikichukuliwa mapema zitapunguza maafa yatokanayo na hali mbaya ya hewa yanayoweza kujitokeza.

Mwisho Dkt. Kijazi aliwatakia wadau wote wa hali ya hewa maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

Siku ya Hali ya Hewa Duniani huadhimishwa tarehe 23 Machi kila mwaka ikiwa ni kumbukizi ya kusainiwa kwa mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).