Na Bolgas Odilo-DODOMA
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema Serikali imeyashirikisha makundi ya anuai za jamii katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili makundi hayo yaendane na maendeleo ya TEHAMA na yanufaike kikamilifu na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia TEHAMA.
Dkt. Ndumbaro amesema hayo March 3,2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha uanzishwaji wa mradi wa ujumuishwaji wa anuai za jamii katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaotekelezwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Dkt. Ndumbaro amesema, uzoefu unaonyesha makundi ya anuai za jamii yasipowekewa mkakati maalum wa kushirikishwa katika uchumi wa kidijitali, mara nyingi yamekuwa yakisahaulika, hivyo Serikali kwa kutambua umuhimu wake imeamua kuyashirikisha rasmi kwenye utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili uwe na tija kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa makundi ya anuai za jamii katika utumishi wa umma hayana mwamko wa kutumia TEHAMA kiutendaji, ila yanalazimika kuitumia kutokana na majukumu waliyo nayo, hivyo changamoto ni kubwa zaidi kwa makundi ya anuai za jamii yaliyo nje ya utumishi wa umma.
Dkt. Ndumbaro amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imeona ni wakati muafaka kwa makundi hayo ya anuai za jamii kushirikishwa kikamilifu ili jamii iweze kwenda pamoja kwenye ulimwengu wa kidijitali.
Akizungumzia mchango wa makundi ya anuai za jamii katika kikao kazi hicho, Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa maoni yao yataisaidia Serikali kutekeleza vema Mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali hasa katika eneo la kuboresha utoaji wa huduma bora kwa umma.
Aidha, ameyashukuru makundi ya anuai za jamii yaliyoitikia wito wa kuhudhuria kikao kazi hicho ili kuiwezesha Serikali kupata maazimio yenye tija kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakati akifunga kikao hicho amesema kuwa mabadiliko ya teknolojia yanagusa maisha yetu ya kila siku katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa Serikali kwa kutambua hili imeweka sera, sheria, kanuni pamoja na kujenga miundombinu ya TEHAMA, kutoa huduma za mawasiliano ili kuhakikisha kuwa wananchi wote pamoja na anuai za jamii zinajumuishwa na kushirikishwa katika TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali
“Kila mmoja wetu atekeleze maazimio mliyokubaliana kwa kuwa taifa hili halina mtu mwingine wa kuliendeleza ila sisi ili taifa letu liweze kuwa mbele na kunufaika na TEHAMA,” amesema Dkt.Yonazi
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Ernest Kimaya ameishukuru Serikali kwa kuwaalika na ameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza vifaa rafiki vya TEHAMA na matumizi yake kwa wananchi hususani kwa anuai za jamii ikiwa ni pamoja na kushirikisha watendaji wa anuai za jamii katika ngazi za kata hadi taifa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI itumike kufikisha na kutekeleza hili.
Naye Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka wazee na kuwajumuisha kwa kuwa wakizungumza katika jamii sauti zao zinasikika kwa kuwa wapo wazee wenye nguvu, utaalamu na hawawezi kuwa nje ya mabadiliko ya teknolojia
Kikao kazi hicho kililenga kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu juu ya ujumuishwaji wa masuala ya anuai za ijamii katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unaotekelezwa na Serikali kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021-2026.