Na Magreth Lyimo na Hassan Mabuye WANMM PWANI

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete ametaka kuheshimiwa kwa mipaka ya ardhi baina ya kijiji na kijiji ili kuepuka migogoro.

 

Alisema, mipaka ya vijiji imewekwa ili kuwezesha utoaji bora wa huduma kwenye jamii husika na wananchi hawapaswi kugombania rasilimali ardhi hiyo. 

 

Ridhiwani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani alisema hayo tarehe 2/3/2022 alipoanza ziara ya  kusikiliza na kutolea ufafanuzi changamoto mbalimbali katika jimbo lake ikiwamo migogoro ya ardhi ambapo katika siku yake ya kwanza  ya ziara yake alitembelea kata ya Miono na kufanya mikutano kwenye Vijiji vitatu vya Kweikonje, Masimbani pamoja na Miono mjini. 

  

‘‘Kila mtanzania ana haki ya kumiliki ardhi sehemu yoyote nchini lakini kwa watu wanaotoka nje ya kijiji husika wanapaswa kufuata sheria na taratibu ikiwamo kuwasilisha maombi ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji na baada ya hapo mkutano mkuu wa kijiji uitwe ili kijiji kiridhie kumpa ardhi hiyo muombaji’’ alisema Ridhiwani Kikwete.

 

Kauli hiyo ya Ridhiwani inafuatia mwananchi mmoja kutoka mkoa mwingine anayeishi kijiji cha Masimbani Kata ya Miono mkoa wa Pwani  kuomba kibali cha kumiliki ardhi katika kijiji hicho na  kuishia kuzungushwa na uongozi wa kijiji. 

 

Katika kikao hicho, ilionekana pia kuna migogoro mingi kati ya wafugaji na wakulima sambamba na migogoro ya mipaka ambapo Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Bi. Lucy Kabyemera alieleza kuwa  kila kijiji ni lazima kipimwe ili mpango wa matumizi bora ya ardhi uweze kuandaliwa alioueleza kuwa utasaidia kuepusha migogoro hiyo ya ardhi.

 

‘‘Kwa kukamilisha zoezi la upimaji haraka itasaidia kuandaa Mpango wa Matumizi bora ya ardhi na kila aliyepimiwa ana haki ya kuandaliwa hatimiliki ya kimila itakayomuhakikishia usalama wa milki yake. Katika zoezi hilo elimu pia itatolewa ili wananchi wajue umuhimu wa kupata hati kwenye  eneo wanayoishi’’ alisema Kabyemera.

 

Mmoja wa wananchi waliohudhuria mikutano hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Bw. Kawambwa alisema kuwa, wananchi wanahitaji kupimiwa maeneo yao ili waweze kupata hati ambazo zitawasaidia kupata mikopo aliyoieleza kuwa itasaidia kuongeza nguvu kwenye biashara zao.

 

Kupitia mkutano huo, wananchi wa Kata ya Maono walisisitizwa pia kutoa ushirikiano, kujitokeza kwa wingi pamoja na kutoa taarifa sahihi kwenye zoezi la Anwani za Makazi linalotegemea kuanza mapema mwezi huu wa tatu 2022 ambapo vijana kwenye mitaa watatumika kukusanya taarifa hizo.