Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo la kufanywa mabadiliko katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwenye ngazi zote za utendaji kazi.

Rais Samia ametoa agizo hilo jana wakati wa hafla ya kupokea Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2020/2021 pamoja na Ripoti ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Ikulu Chamwino, Dodoma.

Rais Samia amesema mabadiliko hayo ni kutokana na Bohari hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hasa katika kuhudumia soko la nchi za Jumuiya ya Maendeleo za Kusini mwa Afrika (SADC).

Vile vile, Rais Samia ameagiza taasisi za Serikali zinazokopa mikopo chechefu kutoka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zirejeshe mikopo hiyo na kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko hiyo.

Wakati huo huo, Rais Samia ameagiza kufanyike ukaguzi na tathmini ya mashirika ya umma na kuyafuta ambayo hayana tija kwa taifa. Mpaka sasa mashirika 38 yanaendeshwa bila Bodi ya Wakurugenzi.

Pia, Rais Samia ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuzisisimamia Halmashauri ipasavyo pamoja na kuwachukulia hatua watumishi wenye matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amaeipongeza TAKUKURU kwa kuweza kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kuitaka Taasisi hiyo kujiielekeza zaidi katika kuzuia kuliko kupambana na rushwa.

Hali kadhalika, amempongeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG ) kwa kuweza kupunguza kiwango cha hati chafu, na kuweza kudhibiti usimamizi wa rasilimali za umma.


Zuhura Yunus

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu