Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

WAZIRI wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa ziara iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Sukuhu Hassan katika nchi za Ulaya na Falme za nchi za Kiarabu hivi karibuni zimeiwezesha Tanzania kusaini mikataba 42 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 19.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwa njia ya mtandao wa zoom na matangazo yake kurushwa moja kwa moja na mitandao mbalimbali ya kijamii wakati akifafanua manufaa yaliyopatikana katika ziara hizo zilizofanyika katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Falme za Nchi za Kiarabu.

Dkt. Nchemba alifafanua kuwa akiwa nchini Ufaransa na Ubelgiji, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alishuhudia utiwaji saini wa mikataba sita yenye thamani ya shilingi za Tanzania trilioni 1.77 na miradi mingine 36 yenye thamani ya shilingi trilioni 17.35 za Tanzania, iliyosainia Dubai, katika nchi za Falme za Kiarabu.

Alisema kuwa mikataba hiyo inahusisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa awamu ya tano wa barabara za mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Euro milioni 178), sekta ya kilimo kupitia Benki ya Kilimo (Euro milioni 81), na msaada wa Euro milioni 425 kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Nchemba alifafanua kuwa hati za makubaliano 36 zilizosainiwa Dubai wakati wa mkutano wa biashara na uwekezaji, zinahusisha hati 12 zilizosainiwa kati ya Wizara na Taasisi za Serikali na wawekezaji mbalimbali katika sekta za umma na binafsi na hati nyingine 23 zilitiwa saini kati ya kampuni binafsi za Tanzania na kampuni binafsi za nje.

Alisema kuwa miradi itakayotekelezwa kutokana na fedha hizo ambazo ni mikopo yenye masharti nafuu na misaada itazalisha ajira zipatazo 200,000 katika kipindi cha miaka minne ijayo itakuwa na manufaa mengi ikiwemo kuongeza wigo wa kodi ya Serikali na kuboresha maisha ya wananchi.

Mjadala huo uliwashirikisha pia baadhi ya mawaziri, akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nishati Mheshimiwa Januari Makamba na Wakuu wengine wa Taasisi za Umma walionufaika moja kwa moja na mikataba iliyosainiwa kutoka pande zote mbili za Muungano, Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.