Na Mwandishi wetu,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amezindua mpango kazi wa kitaifa wa kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu wenye lengo la kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu hapa nchini.

Akizungumza mbele ya wadau mbalimbali wanaochangia kuzui na kupambana biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, Naibu Waziri Sagini amesema kwamba Serikali inataka kuona nguvu kubwa inaelekezwa katika kutokomeza uhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu kwenye kuelimisha jamii hususani vijijini na kwa kuwashirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa.

“Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeokoa watoto, vijana, wasichana na wanawake wengi ambao wangeweza kuwa wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu kama wasingepata elimu husika.” amesema.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo leo, Machi 4, 2022 kwenye uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Nashera, jijini Dodoma.

Aidha Naibu Waziri Sagini amewataka wadau kuhakikisha kwamba kila mmoja anapata nakala ya Mpango kazi huo kwa ajili ya utekelezaji.

Amewaelekeza wataalamu kupitia mpango kazi walioundaa na kubaini kazi watakazozifanyi pamoja na gharama ili kubaini kama fedha zitakazopatikana kutoka serikalini na kutoka kwa wadau.