Marekani na mataifa mengine kumi, yamelaani hatua ya hivi karibuni ya Korea Kaskazini ya kurusha kombora la masafa marefu wakiitaja kuwa kinyume cha sheria na kulitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pia kulaani hatua hiyo kwasababu inakiuka maazimio mengi ya baraza hilo.

Katika taarifa ya pamoja, mataifa hayo 11 yameyahimiza mataifa 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa kutekeleza maazimio yote ya baraza hilo la usalama yanayoiwajibisha Korea Kaskazini kuachana na silaha zake  na mipango ya makombora na kutekeleza vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa.

Awali, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, liliiwekea vikwazo Korea Kaskazini baada ya jaribio lake la kwanza la nyuklia mnamo 2006 na kuvifanya kuwa vikali zaidi baada ya majaribio zaidi ya nyuklia na uzinduzi wa mpango wake wa kisasa wa makombora.