Askari wa vikosi maalumu vya majeshi ya Marekani na Tanzania leo wamemaliza mafunzo ya pamoja (Joint Combined Exchange Training – JCET) ya wiki nane, wakipiga hatua nyingine katika historia ya ushirikiano wa kiusalama kati ya nchi hizi mbili.
Rear Admiral Ramson Godwin Mwaisaka, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji Tanzania, aliongoza hafla ya kufungwa kwa mafunzo hayo iliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Oparesheni za Kulinda Amani, Kunduchi, Dar es Salaam. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mwambata Mwandamizi wa Kijeshi katika Ubalozi wa Marekani, Luteni Kanali Serge Mettes na askari kutoka Kikosi cha Oparesheni Maalumu cha Jeshi la Marekani, Kamandi ya Afrika.
“Tanzania ni kiongozi katika kuhakikisha amani na utulivu katika kanda na tunashukuru kuwa na ubia imara na nchi hii katika masuala ya usalama. Majeshi yetu yana historia ya muda mrefu ya kufanya kazi bega kwa bega na mafunzo haya yaliandaliwa maalumu kuboresha zaidi uwezo wa kufanya kazi pamoja na kuzifanya oparesheni za pamoja kuwa imara zaidi,” alisema Mettes.
Mafunzo haya yaliwaleta pamoja askari wa Vikosi Maalumu vya Jeshi la Marekani na wale wa Vikosi Maalumu vya Wanamaji wa Tanzania katika mafunzo ya wiki nane, wakijifunza pamoja stadi mbalimbali za kijeshi kama vile mbinu za uendeshaji wa kikundi kidogo cha askari, kulenga shabaha, huduma za matibabu, mbinu za medani, Sheria za Migogoro ya Kivita na ulinzi wa haki za binadamu wakati wa vita.
Haya yalikuwa mafunzo ya pili ya pamoja kati ya majeshi ya Marekani na Tanzania katika kipindi cha miezi tisa iliyopita. Kwa mujibu wa Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright, kufanyika mara kwa mara kwa mafunzo na mazoezi haya ya pamoja ni kielelezo cha umuhimu ambao Marekani inauweka katika ushirikiano imara wa kiusalama baina yake na Tanzania.
“Ushirikiano katika nyanja ya usalama ni nguzo ya ushirikiano rasmi kati ya Marekani na Tanzania. Ubia wetu wa miaka 60 umejengwa katika maadili ya pamoja na kuheshimiana, na unaendelea kuimarika siku hadi siku,” alisema Balozi Wright.