Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, leo Machi 4, 2022 wamefutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mbowe na wenzake wameachiwa baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, DPP, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.

Mbowe alikamatwa jijini Mwanza, saa chache kabla ya kuongoza kongamano lililokuwa limeandaliwa na vijana wa Chadema (Bavicha) la kudai Katiba Mpya.

Mara baada ya kukamatwa, alisafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na Jeshi la Polisi kisha kuunganishwa katika kesi ya ugaidi na watuhumiwa wengine watatu, Adam Kasekwa, Halfan Bwire na Mohame Ling’wenya.

Watuhumiwa hao watatu, walikuwa makondamoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikosi 92KJ cha Ngerengere mkoani Morogoro ambao wao walimatwa mwaka 2020.

Mbowe aliyewahi kuwa mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro pamoja na wenzake, walikuwa wakituhumiwa kwa mashtaka matano ya kupanga njama za kufanya ugaidi katika maeneo mbalimbali nchini.

Watuhumiwa hao wote walikutwa na kesi ya kujibu katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam mbele ya Jaji Joachim Tiganga aliyekuwa anaisikiliza kesi hiyo.

Tiganga alikuwa Jaji wa tatu kuisikiliza mahakamani hapo, tangu ilipoanza Septemba 2021 akitanguliwa na Elinaza Luvanda aliyeombwa na kina Mbowe ajitoe naye akakubali kisha akafutia Mustapha Siyani ambaye yeye ajitangaza kujitoa baada ya kuwa ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jaji Kiongozi.