Faru Rajabu amefariki usiku wa kuamkia leo akiwa na umri wa miaka 43.
Faru Rajabu alikuwa mtoto wa faru maarufu aliyejulikana kama Faru John aliyefariki mapema mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 47.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Pascal Shelutete inaeleza kuwa Faru Rajabu alifariki katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na sababu ya kifo chake ikitajwa kuwa ni uzee.
“Sirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) linasikitika kutangaza kifo cha Faru Rajabu wenye umri wa miaka 43 kilichotokea usiku wa kuamkia leo kutokana na sababu ya uzee katika Hifadhi ya Taifa Serengeti” imesema sehemu ya taarifa ya Tanapa
Kwa mujibu wa Tanapa mwili wa faru huyo utahifadhiwa kwa mujibu wa kanuni za asili za uhifadhi.
Faru Rajabu ambaye alizaliwa kwenye eneo Ngorongoro mwaka 1979 na mwaka 1993 alihamia katika Hifadhi ya Serengeti ameacha watoto, wajukuu na vitukuu kadhaa.
Wastaniwa maisha ya faru weusi ambao wako katika kundi la wanyama walio katika hatari ya kutoweka hukadiriwa kuwa kati ya miaka 35 hadi 40.