Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, amesema Sekta ya Uchukuzi iko katika hatua mbalimbali za kushughulikia changamoto za watumishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuongeza tija kwa taasisi hizo.
Naibu Waziri Mwakibete ametoa kauli hiyo alipotembelea karakana ya kutengeneza vichwa na mabehewa ya TRC Mkoani Morogoro na kusisitiza Serikali itaendelea kuwekeza kwenye taasisi hizo ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji nchini.
“Changamoto za kitumishi ambazo zimekuwa zikiendelea hapa nataka niwahakikishie kuwa zitatatuliwa na mtapata mrejesho kupitia viongozi wa taasisi, ninaamini zikishughulikiwa kwa kiasi kikubwa zitachangia mabadiliko kiutendaji” amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu waziri Mwakibete ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wafanyakazi wa karakana hiyo kwa kufanya kazi kwa weledi na kujituma wakiwa na lengo la kuhakikisha kazi hazisimami katika karakana hiyo.
Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewasisitiza watumishi hao kufanya ukarabati wa vichwa na mabehewa kwa kuzingatia thamani ya fedha ili uwekezaji unaofanywa ufanyike kwa makini ili kufanya viendelee kutoa huduma za uhakika na salama.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Albert Magandi, amesema mpaka sasa kupitia watumishi hao wameweza kukarabati vichwa vya treni takribani kumi na Sita kwa ajili kusafirisha mizigo na abiria na vichwa saba kwa ajili ya treni za sogeza.
Naye Mmoja wa watumishi wa karakana hiyo, Bw. Vedastus Lugega, amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo Wafanyakazi wako tayari kuendelea kuhakikisha ukarabati unafanywa kwa wakati na kuzingatia viwango ili kutohujumu Serikali.
Naibu Waziri Mwakibete yuko Mkoani Morogoro kwa ziara ya siku moja kukagua maendeleo ya miradi ya sekta ya uchukuzi ikiwemo mradi wa ukarabati wa vichwa na mabehewa.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)